Ugavi na Manunuzi
Ugavi na Manunuzi
KITENGO CHA USIMAMIZI WA UNUNUZI NA UGAWI (PMU)
Utangulizi
Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi (PMU) kina jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli za ununuzi, ugavi na uondoshaji wa mali za Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Na. 10 ya Mwaka 2023 (Sura ya 410), Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024, pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali. Kitengo kinahakikisha kuwa shughuli zote za ununuzi, ugavi na uondoshaji wa mali zinatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya uwazi, ushindani, usawa, uwajibikaji, ufanisi na thamani halisi ya fedha.
Majukumu ya Kitengo
Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi kina majukumu yafuatayo:
- Kusimamia shughuli zote za ununuzi, ugavi na uondoshaji wa mali za Wizara kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Kanuni zake na miongozo ya Serikali.
- Kumshauri Afisa Masuuli kuhusu masuala yote yanayohusu ununuzi, ugavi na uondoshaji wa mali.
- Kupanga na kuratibu shughuli za ununuzi na uondoshaji wa mali, ikiwemo kuandaa na kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Ununuzi wa Mwaka (Annual Procurement Plan – APP).
- Kupitia mahitaji yanayowasilishwa na Idara Tumizi ili kuhakikisha yanaendana na misingi, viwango na taratibu za ununuzi wa umma pamoja na kupendekeza utaratibu unaofaa wa ununuzi.
- Kuandaa nyaraka za zabuni, matangazo ya zabuni na nyaraka za mikataba pamoja na kuratibu michakato ya ununuzi hadi hatua ya kusainiwa kwa mikataba.
- Kuratibu shughuli za tathmini ya zabuni na majadiliano ya mikataba, kupitia taarifa za tathmini na kuwasilisha mapendekezo ya utoaji wa zabuni kwa Afisa Masuuli au Bodi ya Zabuni.
- Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya ununuzi kwa kushirikiana na Idara Tumizi, ikiwemo kupitia maombi ya marekebisho, nyongeza na mabadiliko ya mikataba na kumshauri Afisa Masuuli ipasavyo.
- Kusimamia shughuli za ugavi, ikiwemo upokeaji, uhifadhi, usambazaji na utunzaji wa bidhaa, vifaa na mali za Wizara.
- Kutunza na kuhuisha rejesta za mikataba pamoja na kumbukumbu za ununuzi, ugavi na mali kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
- Kuratibu matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Kielektroniki (National e-Procurement System of Tanzania – NeST) katika utekelezaji wa michakato ya ununuzi na kuhakikisha taarifa za ununuzi zinaingizwa na kuhuishwa kwa wakati.
- Kusaidia usimamizi wa mali za Wizara kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Mali (Government Asset Management Information System – GAMIS) kwa mujibu wa taratibu za Serikali.
- Kufanya uhakiki wa mara kwa mara wa mali na vifaa, kuandaa taarifa za mali zilizochakaa, zisizotumika au zisizohitajika na kuratibu uondoshaji wake kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
- Kuandaa na kuwasilisha taarifa mbalimbali kuhusu shughuli za ununuzi na ugavi kwa Bodi ya Zabuni, Menejimenti na mamlaka nyingine husika.
- Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na ununuzi, ugavi na uondoshaji wa mali kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, Kanuni zake na maelekezo ya Serikali.