Usajili wa Vituo vya Kulelea Watoto Mchana na Watoto wachanga
UTARATIBU WA USAJILI WA VITUO VYA KULELEA WATOTO WADOGO MCHANA NA WATOTO WADOGO
1.0 Utangulizi
Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, ni moja ya huduma za malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto zinazotolewa katika taasisi zinazoratibiwa na kusimamiwa na Wizara chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii.
Huduma hizi zilianza kutolewa mwaka 1967 wakati wa Vijiji vya Ujamaa kwa lengo la kuwapatia wazazi nafasi ya kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali. Mwaka 1981 ilitungwa Sheria ya vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na mwaka 1982 zilitungwa kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa sheria hiyo ambapo taasisi za serikali ,mashamba makubwa, pamoja na watu binafsi waliazisha huduma hizo ikiwemo; Magereza ,Shirika la reli,mashamba ya mikonge na chai,viwanda vya sukari n.k.
Mwaka 1985 kilianzishwa chuo cha ustawi wa Jamii Kisangara-Mwanga kwa ajili ya kuzalisha walezi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na baadae kupanua wigo kwa watu binafsi na mashirika ya dini kuanzisha vyuo vya malezi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya walezi nchini . Mwaka 2009 ilitungwa Sheria ya Mtoto ambapo Sheria hii iliunganisha Sheria zote zinazohusu watoto ikiwemo sheria ya vituo vya kulelea watoto wadogo mchana.
Huduma hii imegawanyika katika maeneo makuu matatu:
- Vituo vya kulelea watoto wachanga vinavyotoa huduma kwa watoto walio na umri kuanzia miezi 3 hadi miaka 2 (Crèches),
- Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana vinavyotoa huduma kwa watoto walio na umri wa miaka 2 hadi miaka minne (Day Care Centers)
- Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana vinavyomilikiwa na jamii kwa watoto wa umri wa miaka 2 hadi minne (Community Based Day Care Centers).
2.0 Madhumuni ya kuanzisha vituo hivi
Vituo hivi vimeanzishwa kwa madhumuni yafuatayo:
- Kuwapa nafasi zaidi wazazi wa watoto ili waweze kufanya kazi zao za uzalishaji mali bila kuwa na hofu juu ya usalama wa watoto wao wakati wa mchana.
- Kuwapatia watoto mazingira bora yanayowawezesha kukuza akili, mwili, lugha, hisia zao pamoja na kuwakuza kijamii na kiutamaduni.
- Kuwapatia watoto malezi bora,
- Kuwapa mwongozo na mwenendo bora wa maisha, utii, heshima na ushirikiano.
- e)Kubaini na kuendeleza vipaji vya watoto na kuwaandaa kwa ajili ya kujiunga na shule za awali na hatimaye shule za msingi
- f)Kufanya utambuzi wa mapema wa watoto wenye mahitaji maalumu/ ukuaji usio wa kawaida kwa ajili ya kuwapatia afua stahiki.
- g) Kukuza ujifunzaji wa mapema na uhamasishaji wa kila mtoto na kukuza ujuzi wa kukabiliana na changamoto.
3.0 Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia huduma hizi
Huduma hizi zinatolewa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo ifuatayo:-
- Sheria ya Mtoto Sura ya 13 ya sheria za Tanzania Kifungu cha 147-152
- Kanuni za vituo vya kulelea watoto wachanga na watoto wadogo mchana za mwaka 2012;
- Miongozo ya uanzishaji na uendeshaji wa vituo vya kulelea watoto wachanga, watoto wadogo mchana na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana vya Kijamii ya mwaka 2020: na
- Kiongozi cha kitaifa cha mlezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano 2022
- Wizara imeandaa kiongozi cha utengenezaji wa vifaa vya michezo na vifaa vya kujifunzia watoto cha mwaka 2020 ili kuwarahisishia wamiliki wa vituo,walezi pamoja na wazazi kupata mwongozo wa kutengeneza vifaa vya michezo na kujifunzia watoto kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira yetu.
- Pia wizara imeandaa mwongozo wa malezi changamshi ya awali kwa watoto wa mwaka 2008 ambapo mwongozo huu umekuwa ukitumika kutoa mafunzo kazini kwa walezi wa vituo na wazazi katika jamii na kwa sasa tumeweza kuuboresha na kuingiza maeneo ambayo awali hayakuwemo.
4.0 Taratibu za Usajili wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana na Watoto Wachanga
Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 vifungu vya 147 - 152, vinampa Kamishna wa Ustawi wa Jamii mamlaka ya kusajili vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na watoto wachanga. Utaratibu wa usajili ni kama ifuatavyo:
Hatua ya 1:
Mwombaji hutuma maombi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika
Hatua ya 2:
Afisa Ustawi wa Jamii na Afisa Afya hufanya ukaguzi katika mazingira yanayokusudiwa kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa katika kanuni na miongozo ya uanzishaji na uendeshaji na kutoa ushauri wa kitalaam kwa mwombaji na kumshauri mmiliki ipasavyo.
Hatua ya 3:
Endapo mwombaji anazo sifa atajaza fomu (namba 1 kwa kituo cha kulelea watoto wadogo mchana cha binafsi au cha kijamii au fomu namba 2 kwa kituo cha kulelea watoto wachanga) za maombi na kusainiwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri husika pamoja na Afisa Afya. Aidha, taratibu zote zikikamilika Mkurugenzi wa Halmashauri husika atatuma maombi kwa Katibu Mkuu Wizara yenye dhamana na maswala ya Ustawi wa jamii yakiwa yameambatanishwa na nyaraka zifuatazo:
- Fomu namba 1(vituo vya kulelea watoto wadogo mchana) au namba 2(vituo vya kulelea watoto wachanga) zilizosainiwa na kugogwa muhuri na Afisa aliyeruhusiwa kisheria na zilizojazwa kikamilifu.
- Taarifa ya ukaguzi ya Afisa Ustawi wa Jamii na mapendekezo yake
- Taarifa ya ukaguzi ya Afisa Afya na mapendekezo yake.
- Vivuli vya vyeti vya walezi vinavyotambulika na serikali na kuthibitishwa na mwanasheria kuwa ni nakala halisi za vyeti
- Kivuli cha hati miliki ya eneo au mkataba wa upangaji jengo usiopungua miaka 3 uliosainiwa kisheria. Vituo vya kijamii kuwe na uthibitisho wa matumizi ya eneo litakalo tumika
- Hati ya usajili wa taasisi husika isipokuwa kwa kituo kinachomilikiwa na jamii
- Katiba ya shirika endapo mmiliki ni kampuni au asasi isiyo ya kiserikali
- Taarifa za kibenk za miezi 3 isipokuwa kwa vituo vinavyomilikiwa na jamii
- Barua ya utambulisho ya kata kituo kilipo
- Mikataba ya watumishi iliyosainiwa na wanasheria
- Kivuli cha Cheti cha afya cha mpishi kinachotambulika na serikali
Hatua ya 4:
Maombi yatakapo wasilishwa kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii hufanyiwa uchambuzi na endapo mwombaji ametimiza masharti msajili hutoa leseni kwa kituo hicho.
Hatua ya 5:
Endapo mwombaji hajatimiza vigezo huandikiwa barua ya kujulishwa mapungufu kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika.
5.0 Muda wa kukamilisha mchakato wa usajiri kwa mujibu wa sheria
Kanuni 5 (2 – 8) ya Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana, inatoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
Afisa Ustawi wa Jamii ndani ya siku arobaini na tano (45) toka tarehe ya kupokea maombi;
- Atapitia maombi husika na
- Atafanya uamuzi wa iwapo au la maombi husika yamekidhi vigezo vilivyoainishwa chini ya Sheria na kanuni hizi; na
- Atamtaarifu Afisa Afya kufanya ukaguzi stahiki wa majengo ya kituo
- Afisa Afya atafanya ukaguzi kujiridhisha iwapo majengo husika na mazingira ya kiafya yanafaa ndani ya siku ishirini na tano toka tarehe ya kupokea taarifa kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii
- Afisa Ustawi wa Jamii baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi kutoka kwa Afisa Afya atawasilisha maombi husika kwa Kamishna ili kupata kibali chake ndani ya siku kumi na nne (14)
- Pale ambapo Kamishna atajiridhisha kwamba maombi husika yamekidhi matakwa ya Kanuni atatoa cheti cha usajili ndani ya siku ishirini na moja (21) toka tarehe ya kupokea maombi husika
- Pale ambapo maombi hayajakidhi matakwa ya kanuni, Afisa Ustawi wa Jamii atarudisha maombi husika kwa mwombaji ndani ya siku kumi na nne (14), na akiainisha sababu za kutopitisha maombi hayo
- Mwombaji ambaye maombi yake yamekataliwa na kurudishwa, anaweza kuwasilisha upya maombi yake baada ya kutimiza masharti.
- Mwombaji ambaye haridhishwi na uamuzi wa kukataliwa kwa maombi yake atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa Kamishna ndani ya siku thelethini (30) toka tarehe ya kupokea taarifa ya kukataa maombi