Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Mahabusu ya Watoto Tanga

  1.  UTANGULIZI.

Mahabusu ya watoto Tanga ipo Barabara ya 15/16, katika kata ya Usagara ndani ya Tanga Jiji.Mahabusu hii ilianzishwa mnamo mwaka 1965, chini ya Sheria ya mtoto na Vijana Na. 13 Kifungu cha 7(1). Aidha baada ya kutungwa kwa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009, Uanzishaji na uendeshaji wa Mahabusu za watoto nchini unaendeshwa chini ya Sheria hiyo kifungu cha 133(8b)

Watoto wanaopokelewa katika Mahabusu, ni wale ambao wapo chini ya umri wa miaka 18 walioshitakiwa kwa makosa mbalimbali mahakamani, na wamekosa dhamana. Watoto hawa tunawapokea baada ya Mahakama kutoa hati ya kupokelewa katika Mahabusu (Remand warrant/Remand to Retention Home).

Watoto wengine ambao tunawapokea katika Mahabusu yetu ni wale ambao wanakutwa katika mazingira hatarishi na kuhitaji ulinzi na usalama kutokana na ukosefu wa nyumba salama (Safe House).

Watoto wakiwa kituoni tunahakikisha wanahudhuria mahakamani wakati wa kesi zao, na endapo mtoto atahukumiwa kupelekwa katika shule ya maadilisho, Afisa Ustawi wa Jamii atakua na jukumu la kumsindikiza mtoto kama inavyoelekeza kanuni yauendeshaji wa Mahabusu za watoto [Kanuni ya 45 (1&4)].

 

2.0 MAJENGO NA MIUNDOMBINU ILIYOPO.

Mahabusu ya watoto Tanga ina jengo moja ambalo limeunganika na kuwa na mchanganua wa vyumba kama ifuatavyo;

  • Bweni la wavulana lenye vyoo (matundu mawili) na bafu,
  • Bwalo la chakula lenye vyumba viwili kimoja kikitumika kama stoo ya vifaa mbalimbali,
  • Jiko,
  • Bweni la wasichana lenye vyoo(matundu mawili) na bafu,
  • Ofisi,
  • Nyumba ya mtumishi yenye vyumba viwili vya kulala,choo na bafu,sebule na jiko.
  • Kituo kina huduma za maji safi na maji taka lakini pia kina huduma ya umeme.

 

3.0 HUDUMA ZINAZOTOLEWA.

  1. Elimu ya mabadiliko ya tabia.
  2. Kuhakikisha watoto wanahudhuria mahakamani.
  3. Kuwapatia watoto huduma za chakula, malazi, mavazi na matibabu.
  4. Kutoa ushauri nasihi, msaada wa kisaikolojia na afya ya akili kupitia michezo mbalimbali
  5. Elimu ya stadi za Maisha kwa kujifunza kazi mbalimbali za bustani.
  6. Huduma za kiroho.
  7. Msaada wa kisheria (uelewa wa Sheria mbalimbali za mtoto na haki zao)
  8. Kuwapatia ulinzi na usalama.
  9. Kuwafundisha watoto kusoma na kuandika.
  10. Kutembelea /kukutana na familia, kuzitambua na kuwaunganisha watoto na familia zao.

 

Kituo kinatoa huduma sio tu kwa jamii inayotuzunguka bali hata kwa wana jamii wengine ikiwa ni wazazi/ndugu/jamaa ambao wanakuwa wana changamoto za kimalezi kwa watoto wao/wanao walea  kwa kufika kituoni kuomba msaada wa kiushauri na kuwafikisha pia watoto wao kwa ajili ya kuweza kuzungumza nao na kuweza kutambua changamoto za kimalezi ambazo zinaweza kuchangia katika mtoto kuwa mwenye tabia kinzani, hivyo kuchukua hatua ya kufanya nao mazungumzo/kuwarekesha kwa kuripoti kwetu kufuatilia maendeleo yao.

 

4.0 MIRADI ILIYOPO KITUONI.

Kituo cha Mahabusu ya watoto Tanga kwa sasa kinajishughulisha na kilimo cha bustani za mbogamboga kwa ajili ya kazi za watoto waliopo kituoni lakini pia kwa ajili ya matumizi ya lishe kwa watoto waliopo kituoni.