Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Mahabusu ya Watoto Dar Es Salaam

1.0    UTANGULIZI

Mahabusu ya Watoto Dar es salaam ni miongoni mwa Mahabusu sita za Watoto zinazoendeshwa na Wizara. Mahabusu hizo ni Mahabusu ya Watoto: Mbeya, Moshi, Arusha,Tanga na Mtwara. Mahabusu hizo zilianzishwa kwa lengo la kuhifadhi na kutoa huduma kwa watoto waliokinzana na sheria, kushtakiwa katika mahakama za kiraia na kukosa dhamana. Mahabusu hizo huanzishwa chini ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13 Kifungu cha 132(8). Aidha pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Mtoto, Mahabusu za watoto pia huendeshwa kwa kuzingatia Kanuni za Mahabusu za Watoto za Mwaka 2012, Taratibu za Ulinzi na Usalama wa Watoto kwa Shule za Maadilisho na Mahabusu za Watoto za Mwaka 2013, Sera ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto kwa Shule za Maadilisho na Mahabusu za Watoto za Mwaka 2013 na Utaratibu wa Kutoa Malalamiko katika Mahabusu za Watotoza Mwaka 2013. Sheria na Miongozo hiyo imeandaliwa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa watoto na kuhakikisha watoto wanapata huduma zote za malezi, makuzi na maendeleo katika kipindi chote wanapokuwa wamehifadhiwa mahabusu. Huduma katika mahabusu ya Watoto Dar es salaam zilianza kutolewa Mwaka 1962 kwa lengo la kuwapatia Watoto huduma za unasihi, marekedisho ya tabia, elimu, stadi za maisha na ufundi kupitia nyimbo, ngoma na michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaunganishwa na familia zao pale mashauri yao yanapomalizika

 

    1. MISINGI MIKUU INAYOONGOZA MASUALA YA WATOTO WANAOKINZANA NA SHERIA
  1. Marekebisho ya Tabia na kuwaunganisha Watoto na familia au jamii zao
  2. Kuwa na mfumo mbadala wa jinai (kuwepo kwa Mahakama za watoto,mahabusu za Watoto na Program za Marekebisho ya Tabia)
  3. Mazingira rafiki,salama na yenye usiri
  4. Mchakato rafiki wakati wa kushughulikia mashauri yao kuliko mifumo rasmi ya kushughulikia mashauri ya jinai kwa wakubwa ( unifomu,silaha,kupigwa pingu kuwekwa katika vizimba nk hayaruhusiwi)
  5. Kumwezesha mtoto kukubali majukumu na kuwajibika
  1. Adhabu zitolewe kwa lengo na kumrekebisha mtoto na ziwe za muda mfupi

 

3.0 MAHALI ILIPO NA ANWANI

MAHABUSU YA WATOTO UPANGA

BARABARA YA ALYKHAN

S L P 1949

11102  -  DAR  ES  SALAAM

 

3.1 TARATIBU ZA KUWAPOKEA WATOTO

watoto hupokelewa kutoka mahakamani baada ya kukosa dhamana au kushtakiwa kwa makosa ambayo hayana dhamana(capital offences). watoto hupokelewa na walezi na mara baada ya kupokelewa hupatiwa vifaa kama nguo,sabuni,dawa za meno,malapa. kutokana na sababu za kiafya kila mtoto anayepokelewa hunyolewa nywele na kutoruhusiwa kuingia bwenini na nguoalizokuja nazo.mara baada ya kufanyiwa usafi na kuoga watoto hupatiwa kitanda,godoro na mashuka ambapo kila mtoto analala katika kitanda chake (hakuna watoto wanaolala wawili wawili)

 

4.0 HUDUMA ZA MAREKEBISHO YA TABIA ZINAZOTOLEWA KWA WATOTO

Katika kuhakikisha kuwa watoto wanaoshikiliwa katika mahabusu za watoto wanabadilika kitabia, uongozi wa mahabusu unawajibika kuanzisha program mbalimbali za marekebisho ya tabia ili kuwawezesha watoto kuwa na shughuli mbalimbali za kufanya. Sheria ya mtoto, Kanuni ya mahabusu za watoto pamoja na Miongozo mbalimbali inabainisha aina mbalimbali ya shughuli zinazosaidia katika kuwarekebisha watoto hatimaye kuwaunganisha na famila zao

    1. Elimu na stadi za maisha

Watoto wanapo kuwa katika mahabusu za watoto wanahaki ya kupata elimu katika Nyanja mbalimbali. Mfano watoto wanapaswa wafundishwe kwa kuzingatia mitaala inayotolewa na Wizara ya Elimu. Sambamba na hilo watoto wanapaswa kufundishwa haki zao, elimu ya afya ya uzazi na stadi za maisha ili waweze kujitambua. Baadhi yao wanakiri kujifunza na kujua kusoma na kuandika kupitia mahabusu ya watoto, kuandaliwa vizuri kimasomo wakati wa kufanya mitihani ya kitaifa.

4.2 Usafi wa Mazingira

Jitihada zinafanyika kuhakikisha mazingira ya mahabusu yanakuwa safi na salama wakati wowote.Watoto wanafuata ratiba ya usafi binafsi na wa jumla kila siku ikiwemo kufagia,kudeki, kupiga mswaki,  kunyoana nywele, kuoga na kutandika vitanda.

 

4.3 Unasihi na Huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii

Huduma hii ndiyo msingi katika marekebisho ya tabia kwa watoto wanaolelewa siyo tu katika mahabusu za watoto bali katika taasisi zinazotoa malezi ya kitaasisi kama vile Mahabusu za watoto na shule ya maadilisho. Huduma hii ni ya kitaaluma na hutolewa na afisa Ustawi wa Jamii kwa mtoto mmoja mmoja au kundi la watoto

Katika kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki wakiwa mahabusu, huduma za unasihi, msaada wa kisaikolojia na kijamii, uwakilishi mahakamani umeimarishwa Aidha mahusiano na ushirikiano baina yetu na Mamlaka za Serikali za Mitaa kule ambapo mtoto anatoka nao umeboreshwa. Huduma hizi zimewezesha kesi za watoto kuchukua muda mfupi,kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaopata dhamana na kupata idadi kubwa ya wazazi,walezi na ndugu wa karibu wanaofika mahabusu kutembelea watoto. Mchakato wa utoaji wa huduma hii ni kwamba mtoto akipokelewa mahabusu siku inayofuata hufanyiwa uchunguzi wa kijamii wa awali na baada ya mwezi afisa aliyemsikiliza mtoto anaweza kupitia taarifa hiyo na kuiboresha kutokana na taarifa mpya ambazo hutolewa na mtoto. Katika hatua hii watoto hueleza kwa uwazi changamoto zilizowasababishia kujiingiza katika tabia za kihalifu.Afisa aliyemfanyia mtoto tathmini ya mahitaji na tabia hatarishi humwandalia mtoto mpango wa huduma.

 

4.4 Michezo na Burudani

Mtoto awapo mahabusu anahaki ya kushiriki katika michezo mbalimbali ambayo humuwezesha kuchangamsha mwili na akili, kupunguza msongo wa mawazo na huongeza uwezo wa ubunifu katika nyanja mbalimbali.  Aidha watoto kushiriki katika michezo mbalimbali hupunguza muda wa kuwa huru na kukosa muda wa kufikiria masuala mengine ya kiuhalifu. Michezo pia huwezesha watoto kuchoka kimwili na kiakili ambapo wanaposhiriki michezo wanakuwa katika nafasi nzuri ya kulala na kupata usingizi wakati wa usiku.

Mpira ni eneo ambalo watoto wanapenda na wanafurahia.Watoto hucheza mpira mara nyingi kwa kuzingatia ratiba ya kituo. Tumeboresha eneo la michezo ambapo tumekarabati magori kwa ajili ya mpira wa basketball.Kwa kutumia viwanja vya nje watoto hucheza mpira wa miguu na kwa kutumia viwanja vya ndani watoto hucheza basketball.

 

    1. Ufundi, Kilimo na Ufugaji

Huduma hii ni muhimu katika kuibua vipaji na vipawa vya watoto.Ikumbukwe watoto wengi wanaokinzana na sheria ni wale wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao hawakupata fursa ya kwenda shule. Kupitia programu hii watoto hushiriki katika shughuli mbalimbali za ushonaji, ususi, kilimo cha bustani, na ufundi wa aina mbalimbali.

Darasa la ufundi chereheni linaendelea ambapo tuna mwalimu mmoja wa kujitolea ambaye katika kipindi hiki cha likizo anakuja kila siku kuwafundisha watoto. Watoto wameshajua kukata na kushona suruali, magauni, mashati na kaptula. Pia wanaendelea na ufundi wa kutengeneza “culture” pamoja na kufundishana kunyoana nywele, wale wanaojua vizuri wanawaelekeza ambao hawafahamu,hivyo wameweza kujengeana ujuzi kwa namna hiyo.

 

Kwa upande wa Kilimo tumeboresha bustani za mboga ambapo hadi sasa mboga zinapatikana kwa wingi kiasi cha kukidhi mahitaji ya watoto kwa milo yote kwa siku.

 

4.5 Huduma za Kiroho

Huduma hii ikitolewa kikamilifu humwezesha mtoto kujitambua na kuwa na hofu ya Mungu. Pia mafundisho haya humwezesha mtoto kujutia kosa na kumjenga zaidi kuwa kushitakiwa na kuletwa mahabusu siyo mwisho wa maisha yao. Uongozi wa mahabusu unapaswa kuwaalika na kuwakaribisha viongozi wa Madhebebu ya dini (Wakristu na Waislamu) ili wasaidie kutoa huduma hii muhimu. Huduma hii imepewa umuhimu wa pekee kwa kuruhusu viongozi wa madhebebu mbalimbali kufika na kutoa elimu ya dini mara kwa mara. Elimu hiyo hutolewa na viongozi wa dini zote na watoto wote hushiriki bila kujali Imani ya dini zao. Katika kipindi hiki tumejifunza kwamba elimu hii imewasaidia sana watoto kusema ukweli na kukiri juu ya mashtaka waliyoshitakiwa nayo.