Mahabusu ya Watoto Mbeya
Mahabusu ya Watoto Mbeya ni Miongoni mwa Mahabusu tano (5) za Watoto nchini zinazosimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Mahabusu nyingine ni pamoja na Arusha, Upanga-Dar es Salaam, Moshi na Tanga. Mahabusu hizo zilianzishwa kwa lengo la kuhifadhi na kutoa huduma kwa watoto waliokinzana na sheria na kushtakiwa katika mahakama za kiraia na kukosa dhamana.
Mahabusu hii imeanzishwa chini ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Kifungu cha 133(8). Aidha pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Mtoto, Mahabusu za watoto pia huendeshwa kwa kuzingatia Kanuni za Mahabusu za Watoto za Mwaka 2012, Taratibu za Ulinzi na Usalama wa Watoto kwa Shule za Maadilisho na Mahabusu za Watoto za Mwaka 2013, Sera ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto kwa Shule za Maadilisho na Mahabusu za Watoto za Mwaka 2013 na Utaratibu wa Kutoa Malalamiko katika Mahabusu za Watoto za Mwaka 2013. Sheria na Miongozo hiyo imeandaliwa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa watoto na kuhakikisha watoto wanapata huduma zote za malezi, makuzi na maendeleo katika kipindi chote wanapokuwa katika mahabusu.
Huduma katika Mahabusu ya Watoto Mbeya zilianza kutolewa Mwaka 1986 kwa lengo la kuwapatia Watoto huduma za unasihi, marekebisho ya tabia, elimu, stadi za maisha na ufundi kupitia nyimbo, ngoma na michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaunganishwa na familia zao pale mashauri yanapomalizika. Kijiografia Mahabusu ya Watoto Mbeya inapatikana Katika Jiji la Mbeya, Tarafa ya Iyunga, Kata ya Iyela, Mtaa wa Block T na ina ukubwa wa eneo la Hekta 3.6 na inahudumia Watoto kutoka Mikoa yote ya nyanda za juu kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Njombe, Katavi na Iringa. Aidha, baadhi ya Makosa watoto wanayoshtakiwa nayo ni kama vile ubakaji, ulawiti, Wizi, Mauaji, Unyang’anyi wa Kutumia Silaha na Kukutwa na Kusafirisha Madawa ya Kulevya.
Mahabusu ya Watoto Mbeya Mahabusu ina uwezo wa kuhudumia jumla ya watoto 50 kwa wakati mmoja, Watoto wa Kiume 40 na Watoto wa Kike 10.
1.1 MISINGI MIKUU INAYOONGOZA MASUALA YA WATOTO WANAOKINZANA NA SHERIA
- Marekebisho ya tabia na kuwaunganisha watoto na familia au jamii zao;
- Kuwa na mfumo mbadala wa jinai (kuwepo kwa Mahakama za watoto, mahabusu za Watoto na Program za Marekebisho ya Tabia);
- Kuwa na mazingira rafiki na salama kwa Watoto;
- Kuwa na mchakato rafiki wakati wa kushughulikia mashauri yao kuliko mifumo rasmi ya kushughulikia mashauri ya jinai kwa wakubwa (masuala ya kuvaa sare, matumizi ya nguvu -silaha, kupigwa pingu kuwekwa katika vizimba hayaruhusiwi);
- Kumwezesha mtoto kukubali majukumu na kuwajibika; na
- Kuwa na adhabu zinazolenga kumrekebisha mtoto ambazo hutolewa kwa muda mfupi.
2.0 HUDUMA ZINAZOTOLEWA KATIKA MAHABUSU YA WATOTO MBEYA.
Katika kuhakikisha kuwa watoto wanaoshikiliwa katika mahabusu ya watoto wanapata huduma stahiki na wanabadilika kitabia, Wizara inaratibu utoaji wa huduma za msingi na uendeshaji wa programu mbalimbali za marekebisho kama ifuatavyo: -
- Huduma za Msingi
Ili kuhakikisha kwamba watoto wanakuwa na afya na siha njema, Wizara inawapatia huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na; chakula, malazi, matibabu na mavazi.
- Kuhudhuria Mahakamani
Watoto wanaohifadhiwa Mahabusu wanahudhuria Mahakamani kwa mujibu wa ratiba ya Mahakama, hivyo Wizara inahakikisha watoto wanafikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea na mashauri yao ambapo Afisa Ustawi wa Jamii wa eneo husika anakuwepo kuhakikisha maslahi ya mtoto yanazingatiwa wakati wote wa uendeshaji wa shauri la mtoto.
- Elimu
Watoto wanafundishwa kwa kuzingatia mitaala inayotolewa na Wizara ya Elimu na kwa kuzingatia viwango vya elimu, uwezo na mahitaji husika ya mtoto na kuwawezesha kufanya mitihani katika ngazi mbalimbali. Mfano; mitihani ya darasa la saba na kidato cha pili. Sambamba na hilo watoto wanafundishwa haki zao, elimu ya afya ya uzazi na stadi za maisha ili waweze kujitambua na kuwa raia wema. Huduma hii inatolewa kwa ushirikiano na Ofisi za Halmashauri na wadau wa watoto.
- Usafi wa Mazingira
Watoto wanapatiwa maarifa ya usafi wa mwili na usafi wa mazingira ambapo wanafuata ratiba ya usafi binafsi na wa jumla kila siku ikiwemo kufagia, kudeki, kupiga mswaki, kuoga na kutandika vitanda. Huduma hii inawasidia watoto kujua wajibu wao katika kutunza mazingira na afya zao wakiwa Mahabusu na baada ya mashauri yao kumalizika wanapokuwa raia wa kawaida.
- Unasihi na Huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii
Huduma hii ndiyo msingi katika marekebisho ya tabia kwa watoto wanaolelewa katika mahabusu za watoto na katika taasisi zinazotoa malezi ya kitaasisi kama vile Makao ya Watoto na Shule za Maadilisho. Huduma hii ni ya kitaaluma na hutolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kwa mtoto mmoja mmoja au kundi la watoto. Katika kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki wakiwa Mahabusu ya Watoto, Wizara imeimarisha huduma za unasihi, msaada wa kisaikolojia na kijamii, ambapo kwa sasa watoto wote wanapata huduma hizo. Matokeo ya huduma hizi ni kwamba watoto wanaondokana na msongo wa mawazo, wanapata malezi ya kifamilia na kujiona kuwa ni sehemu ya jamii na kuepuka kurudia makosa.
- Michezo na Burudani
Mtoto awapo mahabusu hupata haki ya kushiriki katika michezo mbalimbali ambayo humuwezesha kuuchangamsha mwili na akili, kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza uwezo wa ubunifu katika nyanja mbalimbali kama kuimba, kucheza ngoma, mpira na kuangalia vipindi katika runinga. Aidha, watoto kushiriki katika michezo mbalimbali hupunguza muda wa kuwa huru na kukosa muda wa kufikiria masuala mengine ya kiuhalifu.
- Kilimo
Kupitia program hii watoto hushiriki katika Kilimo cha bustani za mbogamboga ambapo hadi sasa mboga zinapatikana kwa wingi kiasi cha kukidhi mahitaji ya watoto kwa milo yote kwa siku. Kama sehemu ya marekebisho ya tabia, bustani huhudumiwa na watoto wenyewe kuanzia kulima, kumwagilia hadi kuchuma tayari kwa kupikwa. Uzoefu unaonesha Watoto hupokelewa mahabusu wakiwa hawana elimu ya stadi za maisha lakini baada ya mashauri kufungwa wanaondoka wakiwa na ujuzi wa stadi za maisha kama vile kilimo cha mbogamboga ambapo ni faida kwao inayowawezesha kujiajiri na kupunguza uwezekano kurudia makosa.
- Upatikanaji wa Huduma za Kiroho
Huduma za kiroho hutolewa kikamilifu ili kumwezesha mtoto kujitambua na kuwa na hofu ya Mungu. Huduma hizo humwezesha mtoto kutambua kosa, kujutia na kumjenga zaidi kimaadili.
- Kuwaunganisha Watoto na Familia Zao
Katika kuhakikisha watoto wanapata haki ya kuwasiliana na wazazi au walezi wao Wizara inasimamia utaratibu wa kila mtoto kuwasiliana na mzazi au mlezi wake na baada ya shauri kumalizika mtoto huunganishwa na familia yake. Jambo hili hufanyika kwa kuzingatia Kanuni za Mahabusu ya Watoto 2012.
3.0 FURSA ZILIZOPO KITUONI.
Mahabusu ya watoto Mbeya ina fursa zifuatazo;
- Rasilimali ardhi yenye ukubwa wa hekta 1.5 kwa ajili ya miradi ya kilimo ambayo hutumika kulima bustani za mbogamboga na mazao mengine kama vile Maharage, njegere na viazi.
- Wadau wa huduma za Ustawi wa Jamii ambao hutoa misaada mbalimbali kwa wahudumiwa ikiwemo msaada wa huduma za kiroho na misaada ya mahitaji mbalimbali ya huduma za msingi.