Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WANAWAKE, INJINI YA MAENDELEO YA JAMII" - MPANJU

Imewekwa: 06 Mar, 2026
WANAWAKE, INJINI YA MAENDELEO YA JAMII" - MPANJU

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, ametoa rai kwa jamii kuwaona wanawake kama chachu kwa uchumi na injini ya maendeleo ya jamii.

Wakili Mpanju ameyasema hayo, Machi 5, 2026 katika kongamano la kitaifa la wanawake lililofanyika katika ukumbi wa PAPU - Arusha ikiwa ni kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 08, 2026.

Wakili Mpanju amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, elimu, uchumi na maamuzi ya maendeleo kupitia sera, sheria na programu mbalimbali.

Wakili Mpanju ameeleza kuwa mapendekezo yatakayojitokeza katika kongamano hilo yatasaidia kuimarisha juhudi za kitaifa katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, kupambana na ukatili wa kijinsia na kujenga jamii jumuishi yenye fursa sawa kwa wote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) Dkt. Bakari George ameahidi chuo chake kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika mikakati ya kujenga usawa katika jamii.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kupitia Kituo cha Kitaifa cha Utafiti na Uhifadhi wa Machapisho Yahusuyo Wanawake (NWRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) lililoongozwa na kaulimbiu isemayo "Kuhamasisha Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu"