WAZIRI DKT. GWAJIMA ASISITIZA MAGEUZI YA MAENDELEO YA JAMII KUELEKEA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Na Evelina Odemba WMJJWM – Morogoro
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amekabidhi kompyuta mpakato (laptop) kwa Wakuu wa Vitengo vya Maendeleo ya Jamii ngazi ya mikoa ili kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kusisitiza mageuzi ya kada ya Maendeleo ya Jamii kuwa chachu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima amesema hayo leo, Julai 1, 2026, wakati akifungua Kikao Kazi cha Wakuu wa Vitengo vya Maendeleo ya Jamii ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa NSSF mkoani Morogoro.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Gwajima amesema kada hiyo inapaswa kuongoza mabadiliko ya fikra, kujenga mtaji watu na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia ushiriki wa jamii.
Ameeleza kuwa mafanikio ya Maendeleo ya Jamii hayatapaswa tena kupimwa kwa idadi ya shughuli zinazotekelezwa bali kwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi, ikiwemo ongezeko la kipato cha kaya, uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi, uimara wa familia, malezi bora ya watoto na matumizi ya teknolojia katika kuharakisha maendeleo.
Aidha, amewataka viongozi hao kuongoza mapinduzi ya fikra katika jamii kwa kuhamasisha uzalishaji, ubunifu, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali huku akisisitiza kuwa kila Afisa Maendeleo ya Jamii anapaswa kuwa kiongozi wa mageuzi ya jamii badala ya kuwa msimamizi wa shughuli pekee.
Dkt. Gwajima amehitimisha kwa kuwataka Wakuu wa Vitengo hivyo kurejea katika mikoa yao wakiwa na maono mapya ya kuifanya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ionekane kupitia mabadiliko chanya ya maisha ya wananchi kwani historia itawakumbuka kwa mchango wao katika kujenga jamii inayojitegemea, inayozalisha na yenye ushindani katika uchumi wa kisasa.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo mpya wa kada ya Maendeleo ya Jamii katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Wizara itaendelea kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Vitengo vya Maendeleo ya Jamii kwa kuwapatia vitendea kazi, kuongeza matumizi ya teknolojia na kuimarisha uratibu ili kuhakikisha huduma za maendeleo ya jamii zinakuwa zenye ufanisi na matokeo yanayogusa maisha ya wananchi." amesema Maswi