VIJANA WATAKIWA KUTIMIA FURSA ZILIZOPO KWA MAENDELEO YA JAMII.
Na WMJJWM- MWANZA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza ajira kwa vijana pamoja na kupanua soko la ajira nchini.
Dkt. Jingu amesema hayo leo 06 Machi 2036, baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Mwanza na kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Baladya Elkana na kufanya kikao kifupi kujadili fursa mbalimbali za maendeleo ya vijana na wanawake zinazopatikana katika Mkoa huo.
Amesema vijana wanatakiwa kubadili mtazamo kwa kuangalia fursa zinazopatikana katika maeneo yao ili waweze kuendesha shughuli za uzalishaji na kuinuka kiuchumi, huku Serikali ikiwa tayari kuwaunganisha na fursa mbalimbali ikiwemo mikopo ya masharti nafuu.
Ameeleza kuwa hadi sasa Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 13 zimetolewa kusaidia wafanyabiashara ndogondogo lengo likiwa ni kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Baladya Elkana amesema kuwa Halmashauri zote za Mkoa huo zina fursa katika sekta za kilimo, ufugaji na miundombinu, lakini bado baadhi ya vijana hawajazichangamkia ipasavyo.
Alisisitiza umuhimu wa vijana kutambua fursa hizo na kushirikiana na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Aidha, ameongeza kwamba Vijana wanatakiwa kutumia vyuo vya mafunzo ya stadi ikwemo Chuo cha Maendeleo ya jamii Ufundi Cha Misungwi ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuanzisha miradi yenye kuleta utatuzi wa changamoto mbalimbali katika jamii.
Viongozi hao wamewataka vijana wa Mwanza kuwa wabunifu, kutumia mafunzo ya stadi na fursa zilizopo katika halmashauri zao ili kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na ya Taifa kwa ujumla.