Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SERIKALI YASISITIZA UTEKELEZAJI WA ASILIMIA 30 YA ZABUNI KWA MAKUNDI MAALUM.

Imewekwa: 13 Mar, 2026
SERIKALI YASISITIZA UTEKELEZAJI WA ASILIMIA 30 YA ZABUNI KWA MAKUNDI MAALUM.

Na WMJJWM.
MOROGORO

Serikali imeendelea kusisitiza utekelezaji wa kutenga asilimia 30 ya zabuni za umma kwa makundi maalum ili kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo jumuishi nchini.

Akizungumza leo tarehe 13 Machi 2026 Mkoani Morogoro katika ufunguzi wa warsha ya kujenga uwezo kuhusu utekelezaji na uratibu huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema Serikali imeweka utaratibu huo kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410 ya mwaka 2023, unaolenga kutoa fursa za kiuchumi kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

"Hatua hiyo inalenga kuhakikisha makundi hayo yanapata nafasi halisi ya kushiriki katika zabuni za umma, kuongeza kipato chao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa",alisema Dkt.Jingu.

Pia amesema kuwa utekelezaji wa utaratibu huo unaendana na juhudi za Serikali za kujenga uchumi shirikishi unaozingatia usawa wa fursa kwa wananchi wote pamoja na kuendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 (SDGs) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameongeza kwamba kuwepo kwa utaratibu huo bado kuna changamoto mbalimbali zinazokwamisha makundi maalum kunufaika kikamilifu na fursa hizo ikiwemo uelewa mdogo kuhusu zabuni za umma, uwezo mdogo wa kushindana katika zabuni, ukosefu wa mitaji pamoja na taarifa sahihi za masoko.

Kutokana na changamoto hizo, amesema warsha hiyo inalenga kujenga uelewa wa pamoja na kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum.

Aidha Dkt. Jingu ametoa rai kwa taasisi za umma kuzingatia kikamilifu utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum, huku akizihimiza sekta binafsi, mashirika ya kiraia na taasisi za utafiti kushirikiana katika kujenga uwezo wa makundi hayo ili yaweze kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali.
MWISHO .