Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA VIJANA KULINDA MAADILI, KUSHIRIKI MAENDELEO YA TAIFA

Imewekwa: 20 May, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA VIJANA KULINDA MAADILI, KUSHIRIKI MAENDELEO YA TAIFA

Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka vijana nchini kutumia nafasi walizonazo kujenga Taifa lenye maadili, uwajibikaji na maendeleo endelevu badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoharibu mustakabali wao na jamii kwa ujumla.

Dkt. Gwajima amesema hayo Mei 19, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Tanzania (TYDF) lililofanyika katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

Amesema vijana ndio nguvu kubwa ya Taifa, huku akitolea mfano takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinazoonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni zaidi ya milioni 21 sawa na asilimia 34.5 ya Watanzania wote.

Dkt. Gwajima amesisitiza pia kuwa, Maadili mema ni mtaji wa maendeleo, kwani ili kijana aweze kupiga hatua za kimaendeleo hana budi kuwa mwaminifu pale anapoaminiwa katika miradi mbalimbali na kuitimiza kikamilifu hivyo Uadilifu ni mtaji wa fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa vijana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Tanzania (TYDF) na Mkurugenzi Mtendaji wa DOYODO, Rajabu Juma Suleiman, amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwakutanisha vijana, Serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kujadili mustakabali wa vijana nchini na kuweka mikakati ya pamoja ya kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Amesema kupitia TYDF, vijana wamekuwa wakipewa nafasi ya kusikika, kujengewa uwezo kwenye maeneo ya uongozi, elimu, ajira na teknolojia huku wakihamasishwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na uzalendo katika kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi na endelevu.

Mratibu wa TYDF Charles Reuben, amesema kwa kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, kwa kushirikiana na asasi za vijana pamoja na wadau wa maendeleo, wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya vijana 12,900 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji, mafunzo na uhamasishaji wa maendeleo.

Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa wadau kuendelea kuwekeza katika kutatua changamoto zinazowakabili vijana.

MWISHO

slot gacor