SERIKALI KUIMARISHA ELIMU YA MALEZI KUPITIA KAMPASI YA KISANGARA
Na Jackline Minja, WMJJWM
Kilimanjaro
Serikali imesema itaendelea kuimarisha malezi ya watoto na utoaji wa mafunzo ya ustawi wa jamii kwa wananchi ili kupunguza changamoto za misongo ya mawazo, migogoro ya kifamilia na matatizo ya kisaikolojia, sambamba na kujenga jamii yenye maadili mema, ustawi imara na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hiyo katika kutoa wataalamu na elimu kwa jamii kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya watoto pamoja na ustawi wa familia. Amesema hali hiyo inachangia kujenga jamii yenye utulivu na maendeleo endelevu.
“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika eneo la malezi ya watoto na utoaji wa elimu ya ustawi wa jamii kwa wananchi kwa sababu tunaamini kuwa familia imara ndiyo msingi wa jamii imara. Kupitia mafunzo haya tunalenga kupunguza misongo ya mawazo, kuimarisha afya ya akili na kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye maadili mema.” alisema Mahundi.
Aidha, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ustawi wa jamii ili watoe huduma bora zinazokidhi mahitaji ya jamii na kusaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika familia na jamii kwa ujumla.