Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

VIPAUMBELE, BAJETI VIENDANE NA MAHITAJI HALISI YA WATOTO - WAZIRI DKT. GWAJIMA

Imewekwa: 26 Sep, 2026
VIPAUMBELE, BAJETI VIENDANE NA MAHITAJI HALISI YA WATOTO - WAZIRI DKT. GWAJIMA

Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watendaji wa mikoa na halmashauri kujumuisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika mipango na bajeti zao na vipaumbele kwa kuangalia mahitaji halisi ya watoto katika maeneo husika.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Mkutano wa Nusu Mwaka wa Tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) unaifanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 23 - 25, 2026 jijini Dodoma.

Amewaelekeza pia, masuala ya watoto yawe ajenda ya kudumu katika vikao vya mikoa, wilaya na halmashauri, huduma kutolewa kwa namna jumuishi na kuzingatia watoto wenye ulemavu au walio katika mazingira hatarishi.

Amezitaka Halmashauri kusimamia ubora wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, vyenye vigezo stahiki, mafunzo kwa wazazi, walezi na watoa huduma kuimarishwa, pamoja na huduma za lishe na ufuatiliaji wa ukuaji wa mtoto, kuunganisha mifumo ya ulinzi wa mtoto katika utambuzi wa hatari, utoaji wa rufaa na ufuatiliaji wa mtoto na familia.

Amesema, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan nguzo ya Pili inayohusu maisha bora na ustawi wa watu, inatoa wajibu wa kuwekeza katika maendeleo ya binadamu kuanzia hatua za mwanzo kabisa za maisha. Lengo la kuhakikisha watoto wanakua katika mwelekeo stahiki wa maendeleo kufikia umri wa miaka mitano.

"Tukimlea mtoto vizuri leo, tunaiimarisha familia yake. Tukiziimarisha familia zetu, tunaijenga jamii yenye maadili na mshikamano. Na hapo ndipo tutakapojenga Taifa imara, lenye uwezo wa kutimiza Dira ya Maendeleo 2050." amesisitiza Waziri Gwajima.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakimu Chacha Maswi amebainisha kwamba, mkutano huo unaokutanisha washiriki zaidi ya 340 kutoka mikoa, wizara za kisekta, taasisi na mashirika unalenga kufanya tathmini ya Programu hiyo na kupeana uzoefu wa utendaji ili kuwa na mwelekeo wa kwenda mbele zaidi katika kutekeleza Dira 2050.

slot gacor