Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MASWI: WAZEE WASHIRIKISHWE KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Imewekwa: 28 Sep, 2026
MASWI: WAZEE WASHIRIKISHWE KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Na WMJJWM, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikishwaji wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa ili kuhakikisha masuala ya wazee yanapewa nafasi katika mipango ya maendeleo ya nchi.

Maswi amesema hayo  Septemba 23, 2026, baada ya kukutana na viongozi wa Baraza hilo katika Ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Amesema ni muhimu kuimarisha uratibu wa Mabaraza ya Wazee kuanzia ngazi ya Kata hadi Taifa, ili Baraza hilo liwe chombo madhubuti cha ushauri na uwakilishi wa masuala yanayowahusu wazee nchini.

“Nipo tayari kusikiliza na kupokea maoni na changamoto za wazee nchini. Tukubaliane kufanya Baraza kuwa chombo chenye nguvu zaidi na kuweka msingi mpya wa uongozi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050” amesema Maswi.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Taifa lenye ustawi, usawa na maendeleo jumuishi, hivyo malengo hayo hayawezi kufikiwa iwapo wazee wataachwa nyuma katika mchakato wa maendeleo.

Maswi ameongeza kwamba wazee ni hazina ya maarifa, uzoefu na historia ya Taifa, huku wakibeba nafasi muhimu katika malezi, ushauri na kulinda mshikamano wa kijamii.

Aidha ameeleza kwamba Serikali inaendelea kuhakikisha wazee wanapata huduma na ulinzi unaostahili, ikiwa ni pamoja na huduma za afya na bima, ulinzi dhidi ya ukatili, unyang’anyi wa mali na ubaguzi, pamoja na fursa za kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amesema mabaraza hayo yanapaswa kupimwa kwa namna yanavyosaidia kuboresha maisha ya wazee, ikiwemo kuhakikisha wazee wanapata matibabu kwa wakati, wanafikiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii, wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyang’anyi wa mali, pamoja na kusikilizwa kwa hoja na ushauri wao.

Hata hivyo Maswi ametaja maeneo matano ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele katika kuimarisha ustawi wa wazee nchini kuwa ni afya na bima; hifadhi ya wazee; ulinzi dhidi ya ukatili; ushiriki wa wazee katika maendeleo; pamoja na kuimarisha familia na maadili ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazee kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutoa mchango wao katika ujenzi wa jamii yenye amani, utulivu na mshikamano.


Sendo amesema Baraza linaendelea na maandalizi ya shughuli mbalimbali za wazee, ikiwemo maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yatakayofanyika Mkoani Songwe ambapo kaulimbiu inasema "Zama za Maisha Marefu, Tuboreshe Huduma kwa Wazee".
  
MWISHO

slot gacor