WAZIRI MKUU AHIMIZA UZALENDO KWA NGOs
📌 AZINDUA HARAMBEE MFUKO WA NGOs
Na WMJJWM Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanapaswa kuzingatia maadili na uzalendo katika utekelezaji wake wa majukumu kwa kutojihusisha na fedha zitakazoleta uvunjifu wa maadili na uzalendo wa nchi bali kuendelea kudumisha uzalendo na maadili ya taifa.
Mhe. Mwigulu ameyasema hayo wakati wa kilele cha Jukwaa la mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali jijini Dodoma, leo Novemba 27, 2026.
Amesema Serikali inatambua mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa wadau muhimu sana wa maendeleo katika kuwaletea wananchi huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi na kuunga mkono shughuli za NGOs katika kuwaleta wananchi ustawi kupitia utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema mkoa wa Dodoma unaendelea kushirikiana na wadau yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika sekta tofauti kuwahudumia wananchi kwenye maeneo mbalimbali.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema sekta ya NGOs imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma, ajira, na kuwafikia wananchi, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Jamii Ajenda Dira 2025 na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31),
Akitoa salamu za Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) Jasper Makala amesema Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo kupitia utekelezaji wa Ajenda mbalimbali za Serikali ikiwemo utekezaji wa Dira 2050.
Akitoa salamu za wadau Mwakilishi wa Benki ya Stanbic Elias Ngunagwa amesema, wadau wa maendeleo na sekta binafsi wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine, kuhakikisha mchango unaotolewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali unaleta tija katika maendeleo ya jamii.