Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KUHUSU USALAMA WA MTOTO MTANDAONI, AWASISITIZA WAZAZI KUWASIMAMIA WATOTO WAKATI WA LIKIZO

Imewekwa: 28 Nov, 2025
WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KUHUSU USALAMA WA MTOTO MTANDAONI, AWASISITIZA WAZAZI KUWASIMAMIA WATOTO WAKATI WA LIKIZO

WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KUHUSU USALAMA WA MTOTO MTANDAONI, AWASISITIZA WAZAZI KUWASIMAMIA WATOTO WAKATI WA LIKIZO

Na Saidi Saidi WMJJWM - DODOMA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametolea wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wanapotumia mitandao hasa kipindi cha likizo kwani pamoja na maendeleo ya teknolojia kuongeza fursa, yameibua pia hatari mbalimbali kwa watoto.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo alipokutana na watoto wa Shule ya Msingi Martin Luther, mkoani Dodoma, Novemba 26, 2025, ambapo amesema kuwa utafiti wa mwaka 2022 umeonesha kuwa watoto wameendelea kukumbana na ukatili mtandaoni, ikiwemo kushawishiwa kutuma picha zisizofaa na kukutana na wahalifu wanaojificha kwenye majukwaa ya mtandaoni.

Amesema kuwa kutokana na ukweli kwamba watoto hutumia muda mwingi nyumbani wakati wa likizo, matukio ya ukatili huwa katika kiwango cha juu kwa kuwa asilimia 60 ya matukio hutokea majumbani na mara nyingi kuhusisha ndugu wa karibu. Ameishukuru pia Kamati ya Kitaifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni pamoja na wadau mbalimbali kwa jitihada za kuendesha kampeni za ulinzi wa watoto, sambamba na mabadiliko ya sheria muhimu kama Sheria ya Makosa ya Mtandaoni na Sheria ya Mtoto, ambayo yameboreshwa ili kuimarisha usalama wa mtoto katika zama za kidijitali.

Aidha, Waziri Gwajima amewataka wazazi kufuatilia matumizi ya simu na runinga kwa watoto, kuweka muda maalum wa matumizi ya vifaa vya kielektroniki, pamoja na kuwakataza watoto kulala na simu. Pia amesisitiza umuhimu wa watoto kushiriki katika mabaraza na klabu za watoto shuleni ili wajengewe uwezo wa kujilinda dhidi ya hatari za mtandaoni na za kimazingira.

“Watoto, nawaomba msitembee maeneo yasiyo salama hasa nyakati za usiku. Msiwe na mazoea na watu msiofahamu, kwa kuwa siku hizi wapo wengi wasio na nia njema, hususan kwa watoto wa kike. Epukeni kupiga picha zinazoonyesha viungo vya siri na kuzituma kwa watu. Msitoe taarifa binafsi za kwenu au za familia. Na kabla ya kuweka chochote mtandaoni, jiulizeni: ‘Je, wazazi wangu au jamaa zangu wangeona hili, ingekuwa sawa?’” amesisitiza Dkt. Gwajima

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, amewashauri watoto wote nchini kutumia vifaa vya kielektroniki kwa umakini na ufasaha wakiwa nyumbani, hususan kipindi cha likizo ndefu ili kuepusha hatari zinazoweza kuhatarisha usalama wao.

Nao wadau wa maendeleo wanaotekeleza afua za usalama wa watoto mtandaoni wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili, hususan ukatili wa mtandaoni.

MWISHO.