Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WANAWAKE WATAKIWA KUSIMAMA IMARA KATIKA HAKI NA USAWA KUFIKIA DIRA 2050

Imewekwa: 28 Feb, 2026
WANAWAKE WATAKIWA KUSIMAMA IMARA KATIKA HAKI NA USAWA KUFIKIA DIRA 2050

Na Jackline Minja, WMJJWM
Dar es Salaam

Wanawake wametakiwa kusimama imara katika kutetea haki na usawa wao kama msingi wa maendeleo jumuishi ya Taifa kuelekea Dira ya 2050kwa kuwa haki na usawa si upendeleo bali ni hitaji la lazima kwa ustawi wa Taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akifungua kongamano la wanawake kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofikia kilele Machi 8, 2026, lilifanyika katika kanisa la Omega Ministries lililoko Mbezi beach Afrikana mkoani Dar Es Salaam amesema kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050” inalenga kujenga uelewa wa kuwekeza kwa wanawake na wasichana kwa vitendo ili kufikia maendeleo ya kweli na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki zao na fursa sawa.

Alieleza kuwa kufikia dira hiyo kunahitaji wanawake wenye elimu bora na ujuzi wa kisasa, afya njema, fursa sawa za kiuchumi na ushiriki katika maamuzi, huku wasichana wakilindwa dhidi ya ukatili. Akinukuu Zaburi 68:11, amesema, “Wanawake si kundi dhaifu bali ni jeshi la maarifa, ujasiri na matumaini,” akihimiza ushirikiano kati ya wanawake na wanaume katika maamuzi ya kifamilia, kiroho na kimaendeleo.

"kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania, hivyo wana wajibu mkubwa wa kusimamia maadili ya familia na kulea kizazi kijacho na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufungua fursa za kiuchumi na kuboresha miundombinu ya afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto".amesema Mhe. Mahundi