WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA VIKUNDI KAZI VYA UTEKELEZAJI WA MTAKUWWA II
📌📌ATOA MWELEKEO MPYA. UWAJIBIKAJI NA UFUATILIAJI WA HARAKA
Na WMJJWM - Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Vikundi Kazi vya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (MTAKUWWA II), akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji na uwajibikaji ili mpango huo ulete matokeo chanya kwa jamii. Uzinduzi huo umefanyika Februari 27, 2026 katika Ukumbi wa Ofisi za Jiji zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima Amesema licha ya mpango huo kuandaliwa kwa ubora na kupata umiliki wa kisiasa ikiwemo kusainiwa na Mawaziri 16, utekelezaji wake bado ni wa kasi ndogo na uratibu hafifu katika ngazi mbalimbali. Waziri Gwajima amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto hayawezi kufanikiwa bila kila mdau kutekeleza kikamilifu majukumu yake, akitaja changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya uwezeshaji wa uchumi wa kaya, mitandao ya kijamii, mmomonyoko wa maadili na uzingatiaji wa mwongozo wa utoaji adhabu mashuleni.
Aidha, Waziri Gwajima ameagiza kuanzishwa kwa mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa MTAKUWWA II, akieleza kuwa kuanzia sasa kutakuwa na vikao vya tathmini kila baada ya miezi mitatu vitakavyohusisha Wakuu wa Vikundi Kazi na uongozi wa Wizara.
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, amesema utekelezaji wa MTAKUWWA II utahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akizungumza kwa niaba ya mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini amesema wadau wataendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa mchango wa kitaalamu, kifedha na kijamii, ikiwemo kusaidia ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa MTAKUWWA II kwa lengo la kujenga jamii iliyo huru dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.