Habari
WAZIRI GWAJIMA AIPONGEZA CRDB KUWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema programu ya kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi iitwayo iMBEJU iliyoanzishwa na benki ya CRDB itaboresha biashara changa za vijana na wanawake kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara zao, pamoja na mitaji wezeshi.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya programu hiyo kwa wajasiriamali Wilaya ya Ilala kwa mwaka 2023 yaliyowalenga zaidi wanawake na vijana.
Waziri Dkt. Gwajima amesema amefuatilia mchakato wa uanzishwaji na utekelezaji wa programu hiyo ambayo CRDB inashirikiana na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Tume ya TEHAMA (ICTC), ambapo vijana 196 wamepewa mafunzo baada ya mchakato wa awali uliojumuisha vijana wabunifu zaidi ya 700.
"Nimefuatilia pia upande wa uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali, nimeona mkitoa mafunzo katika mikoa na wilaya mbalimbali. Mkurugenzi Mtendaji ameeleza hapa kupitia mafunzo haya tayari program ya iMBEJU imeshawafikia wajasiriamali wanawake zaidi ya 65,000 kupitia mafunzo na tayari mikopo yenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 210 imetolewa." amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza pia programu hiyo inafanya vema kwani imekuwa ikitumia fursa mbalimbali za kuwatengenezea masoko wajasiriamali ambapo hadi sasa zaidi ya 1,000 wamefikiwa na baadhi yao wamepatikana kupitia programu ya iMBEJU.
"Ni imani yangu programu hii itakwenda kuwa mfano kwa programu nyingine za namna hii. Niwahakikishie Wizara yangu itakuwa tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha programu hii inawafikia wanawake na vijana na wengi zaidi."
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema CRDB imeanzisha Programu ya iMBEJU kwa lengo la kutatua changamoto ikiwemo mikopo ya masharti magumu ya taasisi za mikopo ili kuwawezesha wanawake na vijana kukuza mitaji na kuboresha biashara zao
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Vikoba endelevu Semeni Gama, ameeleza kwamba mkopo wa iMBEJU umekuwa ni rahisi sana nanunasadia sana wajarisiliamali wadogo kwani una riba nafuu zaidi.
MWISHO