Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA RASMI BODI YA NNE YA TAASISI YA MAENDELEO YA JAMII TENGERU (TICD)

Imewekwa: 08 Aug, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA RASMI BODI YA NNE YA TAASISI YA MAENDELEO YA JAMII TENGERU (TICD)

Na WMJJWM – Arusha

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka Bodi ya Uendeshaji ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) kuongoza mageuzi ya elimu ya maendeleo ya jamii kwa kuimarisha ubora wa taaluma, tafiti na ubunifu ili kuandaa wataalamu watakaochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akizindua rasmi Bodi hiyo ya Nne Agosti 6, 2026 jijini Arusha

Dkt. Gwajima amesema Serikali imefanya mageuzi ya kimkakati kwa kuunganisha vyuo vinane vya Maendeleo ya Jamii na Maendeleo ya Jamii Ufundi kuwa kampasi za Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kuanzia Julai 1, 2026.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa utendaji, kuimarisha ubora wa elimu na tafiti, pamoja na kuifanya Taasisi kuwa kitovu cha kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto za jamii na kukidhi mahitaji ya Taifa.

Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha Taasisi inaendana na maendeleo ya teknolojia, matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence), pamoja na kufanya mapitio ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira na vipaumbele vya Taifa. Amesisitiza kuwa Serikali inatarajia TICD kuwa kitovu cha elimu, tafiti na ubunifu kitakachochangia maendeleo ya jamii na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), Dkt. John Elton Lusingu, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini Bodi hiyo na kuahidi kusimamia kwa weledi, uwajibikaji na uzalendo utekelezaji wa majukumu yake. Amesema Bodi itashirikiana kwa karibu na Wizara, Menejimenti na wadau mbalimbali kuhakikisha Taasisi inaendelea kuwa kitovu cha ubora katika elimu, tafiti na ubunifu, huku ikiimarisha matumizi ya teknolojia, kuboresha mitaala na kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya Taifa na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

slot gacor