Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

DKT GWAKIMA ASISITIZA UWEKEZAJI KWA WANAWAKE VIONGOZI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Imewekwa: 19 Sep, 2026
DKT GWAKIMA ASISITIZA UWEKEZAJI KWA WANAWAKE VIONGOZI UKANDA WA MAZIWA MAKUU

Dar es Salaam.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema ni muhimu kuwekeza katika kizazi kijacho cha wanawake viongozi nchini Tanzania, katika Ukanda wa Maziwa Makuu na kimataifa, kwa lengo la kutoa fursa na kujenga msingi utakaowaimarisha katika uongozi, usuluhishi, diplomasia, ujenzi wa amani, utawala na ushirikiano wa kikanda.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo, Septemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza katika hafla ya kumtangaza Mgeni Rasmi wa Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), unaotarajiwa kufanyika Novemba 2–5, 2026, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo utawakutanisha wabunge wanawake kutoka nchi 12 za Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu amani, ulinzi, usalama na maendeleo, pamoja na nafasi ya wanawake katika uongozi na ujenzi wa amani.

“Tanzania haijaanza safari yake ya Wanawake, Amani na Usalama leo. Tunajenga juu ya historia ndefu ya wanawake katika ukombozi, ujenzi wa Taifa, diplomasia na ujenzi wa amani. Mkutano huu unatukumbusha kwamba historia pekee haitoshi. Tunapaswa kuhakikisha kuwa historia hiyo inageuka kuwa sera, sheria, bajeti, taasisi na hatua zinazoleta matokeo kwa wanawake na wasichana,” amesema Dkt. Gwajima.

Amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania kunatoa fursa muhimu kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kubadilishana uzoefu kuhusu namna Mabunge yanavyoweza kutumia nafasi zao kuhakikisha wanawake wanashirikishwa na kuwezeshwa katika mipango, bajeti na mifumo ya kitaifa ya uwajibikaji.

Aidha, amesema uongozi wa wanawake nchini Tanzania umejengwa na wanawake waliotangulia katika nyanja mbalimbali, kuanzia katika jamii, siasa na Bunge, hadi Serikali, diplomasia ya kikanda na uongozi wa kimataifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), Balozi Dkt. Deo Mwapinga, amesema Tanzania ni chimbuko la mipango mbalimbali ya amani na usalama katika eneo hilo.

Amesema Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ni zao la Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004, lililoweka msingi muhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kushughulikia masuala ya amani, usalama na maendeleo.

Balozi Dkt. Mwapinga ameongeza kuwa Tanzania inakumbukwa barani Afrika kwa nafasi yake katika harakati za ukombozi wa sehemu kubwa ya Afrika, ikiwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika (Southern Africa Liberation Committee), pamoja na mchango wake katika juhudi za kujenga bara lenye umoja, amani na ustawi.
MWISHO

slot gacor