WAZAZI WAJIPANGE KABLA YA KUAMUA KUWA NA WATOTO, WANAHITAJI MALEZI NA MATUNZO – WAZIRI DKT. GWAJIMA
Na WMJJWMJ - Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wanaume kuwa na dhamira na utayari wa kutimiza wajibu wa malezi na matunzo ya watoto kabla ya kuamua kuwa na watoto, akisisitiza kuwa uzazi unaambatana na jukumu la kuwalea na kuwahudumia watoto.
Ameyasema hayo Septemba 19, 2026, kupitia ukurasa wake wa Instagram wakati akijibu hoja na na maswali mbalimbali ya wananchi.
Dkt. Gwajima amesema baadhi ya wanaume wanapaswa kutafakari kwa kina kuhusu uwezo na utayari wao wa kubeba majukumu ya uzazi, badala ya kuingia katika uzazi bila maandalizi huku akiwataka wanaume wanapotaka kupata watoto kuangalia uwezo au utayari wa kutekeleza majukumu hayo na kufanya maamuzi yanayozingatia ustawi na mustakabali wa watoto watakaopatikana.
Aidha, Dkt. Gwajima amewataka wanawake kutafakari kwa kina kuhusu maandalizi yao ya kielimu na kiuchumi kabla ya kuingia katika mahusiano yanayoweza kupelekea kupata watoto huku akisema ni malalamiko mengi anayoyapokea yanahusu wanawake walioachwa na wenza wao bila kupata matumizi ya watoto, hivyo ni muhimu kuwa na maandalizi ya msingi ya maisha yatakayosaidia kuhakikisha watoto wanaendelea kupata malezi na matunzo hata pale mzazi mmoja anaposhindwa kutekeleza wajibu wake.
Amesisitiza kuwa uzazi ni jukumu linalohitaji maandalizi, uwajibikaji na dhamira ya pamoja kutoka kwa wazazi wote, hivyo kila mzazi anapaswa kutambua wajibu wake na kufanya maamuzi yanayolinda ustawi, malezi na mustakabali wa watoto.