WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA MRADI WA BILIONI 262 KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE - GEITA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akizindua rasmi Mradi wa PAMOJA (Project for Advancing Gender Equality in Tanzania) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyofanyika tarehe 8 Machi 2026 mkoani Geita.
Mradi huo unalenga kukuza usawa wa kijinsia kwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake, kuimarisha juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia pamoja na kuboresha huduma kwa manusura.
Mradi wa PAMOJA unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto Zanzibar.
Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 100, unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unatarajiwa kutekelezwa katika mikoa 10 na halmashauri 40 nchini.
Kupitia mradi huo, wanawake watawezeshwa kiuchumi kwa kuimarishwa kwa vikundi vya kuweka na kukopa, kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara, pamoja na kuwaunganisha na masoko na taasisi za kifedha.
Aidha, mradi utaimarisha kampeni na mifumo ya kupambana na ukatili wa kijinsia, kuboresha huduma kwa manusura, kujenga na kukarabati nyumba salama, pamoja na kuanzisha vituo vya malezi ya watoto katika ngazi ya jamii.