Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA VIJANA KUWA MABALOZI WA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA ‎

Imewekwa: 30 Jun, 2025
WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA VIJANA KUWA MABALOZI WA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA ‎

Dodoma | 24 Juni 2025

‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka vijana kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuelimisha jamii na kusaidia waliopona. Amesema vijana wana nafasi ya kipekee kutumia elimu, ubunifu na ushawishi wao kuleta mabadiliko.

‎Ameeleza kuwa zaidi ya Watanzania 900,000 walihitaji huduma za afya ya akili na tiba ya uraibu mwaka 2023, huku matumizi ya bangi, heroin na cocaine yakiendelea kuongezeka miongoni mwa vijana, yakisababisha magonjwa, uhalifu na kupotea kwa ndoto.

‎Dkt. Gwajima amezitaka taasisi za elimu ya juu kuanzisha programu za elimu na huduma za ushauri kwa wanafunzi. Amesisitiza kuwa mapambano haya yanahitaji nguvu ya pamoja ya serikali, jamii na vijana.

‎“Ninyi si tu viongozi wa kesho, bali wabunifu wa mabadiliko wa leo. Chukueni jukumu hili kwa moyo. Pamoja tunaweza kujenga Tanzania yenye mwangaza,” — Dkt. Gwajima

Naye ‎Waziri wa Nchi (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Ridhiwan Kikwete (Mb) amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua madhubuti kupitia programu kama Mpango wa Kudhibiti Dawa za Kulevya, Mafunzo ya Stadi za Maisha, na huduma za ushauri kwa vijana. Amepongeza wadau na kuahidi kuendelea kushirikiana nao.

‎Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuzuia na kupunguza athari za dawa hizo kwa kutoa elimu, kushirikiana na taasisi, na kutoa huduma za utengamao. Amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kueneza ujumbe wa mapambano.