USHIRIKIANO WA JAMII NI MSINGI WA KUJENGA KIZAZI IMARA - NAIBU WAZIRI MAHUNDI
Na Jackline Minja – WMJJWM
Mbeya
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha malezi katika ngazi ya familia na jamii ili kupunguza idadi ya watoto wanaoingia kwenye mifumo ya haki jinai na kuacha watoto kuishi mitaani.
Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu na utoaji wa huduma katika Mahabusu ya Watoto iliyopo jijini Mbeya, Mhe. Mahundi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda haki za mtoto na kuhakikisha maslahi yao yanazingatiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.
“Dhamira ya Serikali ni kuona mtoto anakua na kulelewa katika familia yenye upendo, ulinzi na maadili mema. Mahabusu ya Watoto ni sehemu ya mwisho na ya mpito, lengo letu kubwa ni kuzuia watoto kufika hapa kwa kuimarisha malezi katika familia na jamii,” amesema Mhe. Mahundi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mussa Mkamate, amesema kuwa ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ni nguzo muhimu katika malezi ya watoto na mustakabali wa taifa.
“Watoto wanahitaji malezi chanya, uangalizi na upendo kutoka kwa familia na jamii. Tukishirikiana kwa pamoja, tutaepuka kuwa na watoto wengi mitaani na kujenga kizazi imara kitakacholilinda na kulijenga taifa,” amesema Mkamate.
Naye Meneja wa Mahabusu ya Watoto Mbeya, Reuben Ndelembi, ameeleza kuwa Mahabusu hayo kinaendelea kutoa huduma za marekebisho ya tabia, msaada wa kisaikolojia, elimu ya stadi za maisha pamoja na kuwaunganisha watoto na familia zao pindi mashauri yao yanapokamilika.
Ziara hiyo ya Mhe. Mahundi ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia na kutathmini utoaji wa huduma katika vituo vya ustawi wa jamii, huku ikisisitizwa kuwa ulinzi na malezi ya watoto ni jukumu la kila mmoja kwa ajili ya kujenga taifa lenye maadili na kizazi chenye msingi imara.