SHULE ZA MAADILISHO NI FURSA YA PILI KWA WATOTO WALIOKINZANA NA SHERIA - MHE.MAHUNDI
Na Jackline Minja – MJJWM, Mbeya
Watoto waliokinzana na sheria na kupelekwa katika Shule ya Maadilisho ya Irambo iliyopo Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya wamehimizwa kujutia makosa yao, kubadili mienendo na kuishi kwa utii na maadili mema mara baada ya kumaliza adhabu na kurejea katika jamii walizotoka.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum , Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto waliokinzana na sheria wanarekebishwa kimaadili na kisaikolojia.
“Hii ni fursa ya pili mliyopewa na Serikali itumieni kujitathmini, kujutia makosa na kuamua kubadilika ili mtakaporejea katika jamii muwe mfano wa kuigwa maana mnajua kabisa kutowasikiliza wazazi na jamii kumewasababisha wengi wenu kujiingiza katika vitendo vinavyopingana na sheria na hatimaye kujikuta mmefikishwa katika shule hii na naamini ndani ya miaka hiyo uliyopangiwa na Serikali naamini itawasaidia kubadilika” amesema Mhe. Mahundi.
Aidha, aliwasisitiza watoto hao kuwa utii, nidhamu na maadili mema ni nguzo muhimu zitakazowawezesha kujenga maisha bora na kuepuka kurudia makosa ya awali, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya malezi katika shule za maadilisho nchini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Mhe. Patali Shida Patali, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hilo, pia kukifanya kituo hicho kuwa katika jimbo lao ambapo kinasaidia watoto wa vijiji vyao na Tanzania nzima.
“Mheshimiwa Naibu Waziri kuwepo kwa kituo hiki sisi Mbeya Vijijini tunanufaika kwani tuna mahusianao mazuri na kituo hiki kwa kuwa kinatunufaisha katika masuala mbalimbali ikiwemo maji tunapata kwao, elimu za mashamba darasa tunazipata hapa pamoja na huduma za afya wanakijiji hutumia zahanati ya shule hii” amesema Mhe. Patali.
Awali akisoma taarifa ya shule hiyo, Meneja wa Shule ya Maadilisho Irambo John Meshack amesema kuwa, shule hiyo kwa sasa inahudumia watoto 28 wa kiume waliotoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na watoto hao wanapatiwa huduma muhimu ikiwemo elimu ya msingi, afya, stadi za maisha, malezi na michezo kwa lengo la kuwabadilisha tabia na kuwaandaa kurejea katika jamii wakiwa raia wema.
Ziara ya Naibu Waziri Mahundi inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa kisiasa na taasisi za malezi katika kuhakikisha watoto waliokinzana na sheria wanapata marekebisho stahiki na kurejeshwa salama katika jamii.
MWISHO