WAZIRI DKT. GWAJIMA AWAONYA WASIMAMIZI WA MIRATHI WANAODHULUMU WARITHI
Na WMJJWM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewaonya watu wanaopewa dhamana ya kusimamia mirathi ya marehemu na kutumia vibaya nafasi zao kwa kujimilikisha mali za marehemu kinyume na sheria, akiwataka kutimiza wajibu wao kwa haki na kwa wakati.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, leo Oktoba 18, 2026 Dkt. Gwajima amesema baadhi ya wasimamizi wa mirathi wamekuwa wakipindisha taratibu kwa kutumia mali za marehemu kwa manufaa yao binafsi au kujimilikisha kabisa, hali inayosababisha migogoro ya kifamilia na kuongezeka kwa kesi za mirathi.
Ameeleza kuwa vitendo hivyo vinawaathiri warithi, wakiwemo watoto wanaoweza kukosa mahitaji muhimu na fursa ya kupata elimu wakati mali za wapendwa wao zikiwa chini ya usimamizi wa watu wanaoshindwa kutimiza wajibu wao. Amewataka wasimamizi hao kuacha vitendo hivyo na kuhakikisha mali za marehemu zinasimamiwa kwa mujibu wa sheria na haki za warithi zinazingatiwa.
Aidha, Dkt. Gwajima amewahimiza watu wanaodhulumiwa katika masuala ya mirathi au wanaobaini kuwa wasimamizi wa mirathi hawatekelezi wajibu wao ipasavyo kutoa taarifa mapema ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kabla mali hazijapotea au kutumika vibaya.
Katika ujumbe huo, amesisitiza pia umuhimu wa watu kuandika wosia wakiwa hai ili kuweka wazi namna mali zao zitakavyosimamiwa na kurithiwa baada ya kifo, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza migogoro ya kifamilia na wingi wa kesi za mirathi.