Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA ATAKA USHIRIKIANO WA SERIKALI NA NGOs UIMARISHWE ZAIDI ILI KUFIKIA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Imewekwa: 15 Jul, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA ATAKA USHIRIKIANO WA SERIKALI NA NGOs UIMARISHWE ZAIDI ILI KUFIKIA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Na Saidi Saidi WMJJWM, Dodoma,  

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kupitia ubia wa kimkakati unaolenga kuleta mabadiliko halisi katika maisha ya wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo Julai 14, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi kati ya Wizara na viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhusu ushirikiano wa kimkakati kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 huku akisema Mashirika hayo ni wadau muhimu wa maendeleo na yanapaswa kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na jamii katika kutekeleza vipaumbele vya Taifa kwa mwelekeo mmoja.

Aidha, Dkt. Gwajima ameyataka mashirika hayo kujielekeza katika utekelezaji wa miradi yenye matokeo yanayopimika katika maisha ya wananchi, ikiwemo kuongeza kipato, kupunguza umaskini, kuboresha lishe ya watoto, kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuongeza uwezo wa vijana kujiajiri. Amesisitiza kuwa mafanikio ya miradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya semina, warsha au mikutano iliyofanyika, bali kwa mabadiliko halisi yaliyoletwa katika maisha ya wananchi.

Vilevile, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zinapaswa kuongozwa na mahitaji halisi ya Watanzania na vipaumbele vya Taifa, sambamba na kutumia teknolojia za kidijitali, data, tafiti na akili mnemba katika kuboresha huduma za kijamii.

Pia ameyataka Mashirika hayo kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika kubuni, kumiliki na kusimamia miradi ya maendeleo ili matokeo yake yawe endelevu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakimu Chacha Maswi amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia katika utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala, amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yataendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa vipaumbele vya Taifa na miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwa Mashirika hayo yako tayari kuimarisha ushirikiano na Serikali ili kuchangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

slot gacor