Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI UTEKELEZAJI, SERA YA TAIFA YA JINSIA

Imewekwa: 16 Jul, 2026
WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI UTEKELEZAJI, SERA YA TAIFA YA JINSIA

Na Oscar Tarimo WMJJWM Morogoro

Maafisa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E), Maafisa Mipango na Waratibu wa Masuala ya Jinsia wametakiwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023.

Hayo yamesemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Hanipher Kilua, wakati akihitimisha warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na UN Women, kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland ikiwa na lengo kuwajengea uwezo maafisa hao iliyofanyika mkoani Morogoro, Julai 14 na15, 2026.

Hanipher amesisitiza umuhimu wa ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa zenye ubora ili kuwezesha maamuzi yanayozingatia ushahidi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera hiyo katika sekta mbalimbali ambapo Wizara kwa kushirikiana na Shirika la UN Women wameandaa mwongozo wa kusimamia na kuratibu masuala ya  jinsia pamoja na kuandaa madawati ya usawa wa kijinsia nchini ambayo moja kwa moja yanagusa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023.

Aidha, amesema, utekelezaji madhubuti wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake kupitia mipango kazi ya sekta utachangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia, inayotoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume, na inayochochea maendeleo endelevu nchini.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Sera na Uratibu wa Masuala ya Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Jinsia (UN Women), Adolphina Mbekenga, amesema warsha hiyo imeimarisha uwezo wa washiriki katika ufuatiliaji, uchambuzi na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Sera hiyo, hivyo UN Women itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wa maendeleo katika kuimarisha mifumo ya uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya masuala ya jinsia ili kufanikisha malengo ya maendeleo.

Naye Afisa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Aren Gregory Werema amesema Wizara hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia kwa wanafunzi mashuleni, wananchi kupitia makundi mbalimbali ya jamii, pamoja na viongozi na wanasiasa inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao kwa kuzingatia sheria za nchi na misingi ya usawa wa kijinsia, sambamba na kuhamasisha ushiriki mpana katika michakato ya uongozi na uchaguzi.

Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,  Wizara ya Afya, Wizara ya Maji ,Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

slot gacor