SERIKALI IMETENGA BILIONI 1 UKARABATI MAKAZI YA WAZEE NCHINI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI
Na Jackline Minja, Kigoma
Serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya kuishi kwa wazee nchini kupitia uboreshaji wa Sera, huduma za afya na ukarabati wa makazi ya wazee ili kuhakikisha wanaishi kwa heshima, usalama na utu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, Julai 14, 2026, alipotembelea Makazi ya Wazee na Wasiojiweza Kibirizi mkoani Kigoma kwa lengo la kujionea hali ya utoaji wa huduma za ustawi wa jamii kwa wazee wanaoishi katika makazi hayo.
"Serikali inatambua wazee kuwa ni tunu, hazina ya hekima na msingi wa maadili ya Taifa letu. Tunathamini mchango wao mkubwa katika ujenzi wa familia, jamii na Taifa, hivyo tutaendelea kuhakikisha wanaishi kwa heshima, usalama na utu, Makazi ya wazee yanapaswa kuwa suluhisho la mwisho pale ambapo mazingira ya kifamilia hayatoi fursa ya kuwahudumia wazee, huku jamii ikiendelea kuthamini na kuwalea wazee ndani ya familia zao " alisema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee nchini, ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 100 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha Makazi ya Wazee Kibirizi ili kuendelea kuwapatia wazee mazingira salama na huduma bora zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, amewapongeza watumishi wanaotoa huduma katika Makazi ya Wazee Kibirizi kwa kujitolea kuwalea na kuwahudumia wazee kwa upendo na heshima na kuhakikisha vituo hivi vinakuwa sehemu salama ambapo wazee wanaishi bila unyonge na wanapata huduma zote stahiki
“Hii ni Wizara inayogusa moja kwa moja maisha na utu wa wananchi niwapongeza watumishi wote wa makazi haya kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwalea na kuwahudumia wazee wetu, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha vituo hivi vinakuwa sehemu salama ambapo wazee wanaishi bila unyonge na wanapata huduma zote stahiki