WAZIRI DKT. GWAJIMA ASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA VIONGOZI WA WIZARA.
WAZIRI DKT. GWAJIMA ASISITIZA UWAJIBIKAJI KWA VIONGOZI WA WIZARA.
Na Jackline Minja WMMJWM-Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka viongozi wa Wizara hiyo kuwajibika katika utekekelezaji wa majukumu yao kimkakati ili kuwahudumia wananchi kwa maendeleo na ustawi wao.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi hiki ni jukwaa muhimu la kutafakari kwa Kikao kazi cha Mkakati kwa Viongozi hao kilichofanyika tarehe 30 Januari, 2026 jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Sukuhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na jamii kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa Menejimenti ya Wizara ina jukumu kubwa la kuhakikisha sera, mipango na maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayoonekana.
“Ninapenda kusisitiza kuwa, mafanikio ya Wizara yetu yanategemea sana namna tunavyosimamia rasilimali tulizopewa, hususan rasilimali watu na fedha. Tunapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo, kuimarisha nidhamu ya kazi, uadilifu na kuepuka urasimu usio wa lazima unaokwamisha utekelezaji wa majukumu yetu.” Amesema Waziri Gwajima
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amehimiza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa viongozi kama menejimenti, Mawasiliano ya wazi, kufanya kazi kwa timu na utatuzi wa changamoto kwa pamoja ni msingi muhimu wa kuleta tija katika utendaji wetu wa kila siku.
“Natarajia kikao kazi hiki kitaibua hoja muhimu, kujadili changamoto kwa uwazi na hatimaye kutoa maazimio ya wazi, yanayotekelezeka na yatakayofuatiliwa ipasavyo. Ni matarajio yangu kuwa maazimio yatakayofikiwa yatachochea ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara/Taasisi zetu.” Amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema Menejimenti hiyo itajikita katika maazimio ya Kikao kazi hicho ili kuongeza kazi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Kikao hicho kimejumuisha Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Taasisi, Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Makamu Wakuu wa Taasisi, Makamu Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
MWISHO