WAZIRI DKT. GWAJIMA APONGEZA JITIHADA ZA WANANCHI, UJENZI ZAHANATI MAGOYE
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Makete, Njombe
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewapongeza wananchi wa kata ya Itundu, Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kushirikiana na Serikali, kujenga na kukamilisha Zahanati kwenye Kijiji cha Magoye.
Waziri Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi wa Zahanati hiyo Julai 7, 2026 amesema, wananchi wanapaswa kujiepusha na taarifa potofu zinazotolewa na watu wasiolitakia mema Taifa, badala yake watafute taarifa sahihi kuhusu fursa za uwezeshaji kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo, pamoja na kufuata taratibu na ngazi sahihi za kutatua changamoto wanazokutana nazo katika kuzifikia fursa hizo.
Aidha, Dkt. Gwajima ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya huduma za afya hadi vijijini pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na huduma bora za matibabu.
Pia Dkt. Gwajima ametoa wito kwa viongozi kuanzia ngazi ya vijiji, kata na halmashauri kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa karibu na wananchi kwa kuwapatia elimu sahihi, ushauri na mwongozo kuhusu namna ya kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Gwakisa, kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo, amemshukuru Dkt. Gwajima kwa kuzindua Zahanati huku akisema uongozi wa Wilaya ya Makete umepokea maagizo hayo na uko tayari kuyatekeleza kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi zote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kunufaika kikamilifu na fursa zinazotolewa na Serikali.
Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi 139,000,000, ambapo wananchi wamechangia shilingi 7,620,000, kwa kushirikiana na Mfuko wa TASAF. Ujenzi huo umehusisha jengo la zahanati, vyoo vya nje, kichomea taka, mnara wa tenki la maji safi, pamoja na ununuzi wa samani na vifaa tiba.
MWISHO