WAZIRI DKT GWAJIMA AITAKA TAHILISO KUTOA ELIMU YA KUZIJUA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANAFUNZI
Na WMJJWM – Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameutaka uongozi Jumuiya ya Wanafunzi, Taasisi za elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO) kuhakikisha wanaandaa makongamano ya kuelimisha vijana kuzijua fursa na kubadili mitazamo hasi ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Septemba 18, 2026 jijini Dar Es Salaam wakati akizungumza na wajumbe wa Jumuiya hiyo.
Dkt. Gwajima amesema Jumuiya hiyo ina nafasi ya kuwaelimisha vijana wanaojiunga na vyuo mbalimbali nchini kuzijua fursa zinazotolewa na Serikali amabazo zinalenga kuwainua kiuchumi na kuharakisha maendeleo yao wakiwa chuoni au baada ya kuhitimu.
“Moja ya changamoto kwa vijana wetu wengi wanakosa sifa za kuaminika na taasisi za fedha pamoja na kukosa taarifa sahihi, hivyo nawaomba ninyi kuwa msitari wa mbele katika kutoa elimu ya fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali pamoja na sekta binafsi”amesema Dkt Gwajima.
Aidha Dkt. Gwajima ameeleza kwamba vijana wengi wanapoingia vyuoni hukumbana na changamoto za makundi rika ambazo huwapotezea mwelekeo wa kielimu na maisha, hivyo zinahitajika jitihada za makusudi za kuwapa elimu ya kujitambua na kuzingatia malengo ya kimaisha wakiwa bado wapo chuoni.
Ameongeza kwamba TAHILISO inatakiwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya madawati ya jinsia vyuoni ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia vyuoni.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jumuiya hiyo Beatrice mwahegili amesema wataendelea kuhimiza wanafunzi vyuoni kuzijua fursa za kiuchumi kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi wawapo vyuoni au wanapohitimu Ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine.