Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AHIMIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI, AKABIDHI MAJIKO YA GESI 544 MCHINGA

Imewekwa: 23 Nov, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA AHIMIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI, AKABIDHI MAJIKO YA GESI 544 MCHINGA

Na WMJJWM, LINDI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati chafu. Amesema takribani watu bilioni 2.1 duniani wanategemea nishati chafu kwa ajili ya kupikia, huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zikionesha kuwa matumizi ya nishati hiyo yalisababisha vifo vya takribani watu milioni 2.9 mwaka 2021.

Akizungumza Novemba 22, 2026, katika hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi 544 kwa wajumbe wa Mabalozi wa Shina wa Jimbo la Mchinga, iliyofanyika katika Kata ya Milola, mkoani Lindi, Dkt. Gwajima amesema changamoto ya matumizi ya nishati isiyo safi inahitaji ushirikiano wa Serikali, viongozi wa jamii, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa nchini Tanzania ni asilimia 16 pekee ya wananchi wanaotumia nishati safi ya kupikia, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kubadili mifumo ya upikaji ili kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu. Amesisitiza kuwa wadau mbalimbali wanapaswa kushiriki katika juhudi za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati safi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Mhe. Salma Kikwete, amesema ugawaji wa majiko hayo ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, inayokwenda sambamba na juhudi zinazofanywa na Serikali. Ameeleza kuwa katika awamu mbili za kampeni hiyo, Jimbo la Mchinga limefanikiwa kugawa jumla ya majiko ya gesi 1,288 kwa wananchi.

Baadhi ya wajumbe wa Mabalozi wa Shina waliopokea majiko hayo wamemshukuru Mbunge kwa msaada huo, wakieleza kuwa utawasaidia kutumia nishati safi katika shughuli zao za kila siku za upishi na kupunguza utegemezi wa nishati chafu. Wamesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati katika kaya na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kupikia kwa kutumia nishati safi.

slot gacor