WAZIRI DKT. GWAJIMA AGAWA SIMU KWA MAAFISA USTAWI WA MIKOA YOTE 26 NCHINI ILI KUFIKIA JAMII KWA WEPESI
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amegawa Simu Janja kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha ukaribu wa maafisa hao na wananchi kupitia fursa ya mawasiliano ya kisasa. Hatua hiyo inalenga kurahisisha wananchi kuwafikia maafisa hao na maafisa kuwafikia wananchi hivyo, kurahisisha uratibu wa huduma za ustawi wa jamii katika ngazi ya mikoa.
Dkt. Gwajima amegawa Simu hizo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 31 wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO), ulioanza Machi 24 na kuhitimishwa Machi 26, 2026 jijini Dodoma. Mkutano huo umewakutanisha wataalamu na Maafisa Ustawi wa Jamii zaidi ya 400 kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, ukilenga kujadili namna ya kuboresha utoaji wa huduma za ustawi wa jamii nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Gwajima amesema ugawaji wa simu hizo ni mpango endelevu utakaofika mpaka ngazi ya wilaya zote na ni utekelezaji wa falsafa ya KAZAKAZAWA (Kasi Zaidi, Karibu Zaidi na Wananchi), inayolenga kuongeza ukaribu wa huduma za ustawi wa jamii na wananchi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano.
“Simu hizi zimesajiliwa kwa jina la wizara na kugharamiwa uendeshaji wake ziwasaidie kutatua changamoto za wananchi kupitia teknolojia ya mawasiliano ya kidigitali kama alivyoahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dktm Samia Suluhu Hassan na kuelekeza kwamba, wakati wote serikali iwe karibu zaidi na wananchi, niwaombe tukaweke bidii kuwafikia wananchi nasi watufikie” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Wakili Amon Mpanju, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kutumia vifaa walivyokabidhiwa kwa kuzingatia weledi, maadili ya kazi na uwajibikaji mkubwa ambapo, wizara itakuwa inalipia gharama za mawasiliano hayo.
Nao wataalamu wa ustawi wa jamii wameishukuru Serikali kwa kuwapatia vifaa hivyo na kugharamia uendeshaji wake, wakisema, vitarahisisha kazi ya kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.