WAZIRI DKT. GWAJIMA AAINISHA VIPAUMBELE VITANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII 2025/2026.

Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii. Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameainisha vipaumbele vya Wizara vikubwa vitano katika utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mhe. Dkt. Gwajima ameainisha hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka husika wa Fedha leo Mei 27, 2025 Bungeni jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa Wizara kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake zitatekeleza vipaumbele hivyo ambavyo ni kukuza ari ya Jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ngazi ya msingi, kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za ustawi wa maendeleo ya jamii, kutambua pamoja na kuratibu maendeleo ya ustawi kwa Makundi Maalum.
Mhe. Dkt. Gwajima ameongeza kuwa vipaumbele vingine ni pamoja kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.
Amesema Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo katika Ngazi ya Msingi (2022/23 – 2025/26) ambao unalenga kuwawezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo na kuchochea mageuzi ya kifikra, mtazamo na kiutendaji kwa timu ya wataalam ngazi ya msingi ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika kuhakikisha Watoto wanalindwa na ukatili Waziri Dkt. Gwajima amesema Wizara imeratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection - COP) katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara. Kampeni ilikuwa na lengo la kuelimisha Wazazi au Walezi na Watoto wenyewe kuhusu Usalama wa Mtoto anapokuwa anatumia mitandao.
Aidha Mhe. Dkt. Gwajima amefafanua kuwa Wafanyabiashara ndogondogo 601 (Me 274; Ke 327) wamekopeshwa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1,101,650,000 na zoezi hilo linaendelea. Vilevile maombi 2,092 yanaendelea kuchakatwa yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3,590,477,000.