Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZEE WAASWA KULINDA MAADILI NA AMANI YA TAIFA

Imewekwa: 05 Nov, 2026
WAZEE WAASWA KULINDA MAADILI NA AMANI YA TAIFA

Na Evelina Odemba

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Abubakar Kunenge, amewataka wazee nchini kuendelea kutumia hekima na busara zao kulinda maadili, mila na desturi za taifa, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kudumisha amani na mshikamano wa jamii.

Kunenge amesema hayo Novemba 5, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Songwe, ambapo amewahimiza wazee kuwa na subira na kuendelea kutoa ushauri wenye kujenga kwa viongozi na jamii.

“Wazee, mna hekima kubwa. Ninyi ni walinzi wa mila na desturi za taifa letu, tunajifunza kwenu. Taifa hili linawatambua na kuwategemea,” amesema Kunenge.

Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwataka viongozi katika ngazi zote kuhakikisha wanashughulikia changamoto zinazowakabili.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Ushauri Taifa, David Sando, amesema wazee wameazimia kulinda maadili ya jamii na kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, huku akiwataka wenzao kuepuka lugha za uchochezi, matusi na dhihaka dhidi ya viongozi.

“Viongozi hawa ni watoto wetu na ni hazina ya taifa letu, tuwashauri kwa hekima, busara na upendo,” amesema Sando.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, amesema Serikali inaendelea kuimarisha ustawi wa wazee kwa kuboresha huduma za afya na makazi.

Amesema kupitia bajeti ya mwaka 2026/2027, Serikali imepanga kujenga makazi nane ya kisasa ya wazee katika kanda mbalimbali nchini, sambamba na kutumia mfumo wa kielektroniki kukusanya taarifa za wazee ili kuboresha upangaji wa bajeti na utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji yao.

MWISHO

slot gacor