SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUIMARISHA USTAWI WA WAZEE NCHINI
Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha mifumo na huduma za kijamii zinazolenga kuboresha ustawi wa wazee nchini, ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za afya, makazi salama na mazingira wezeshi yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Ahadi hiyo imetolewa Novemba 4, 2026, na Naibu Katibu Mkuu, Wakili Amon Mpanju, aliyewasilisha salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika Kongamano la Wazee mkoani Songwe.
Wakili Mpanju amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa, akibainisha kuwa kundi hilo ni hazina muhimu ya uzoefu, maadili na maarifa yanayopaswa kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ameongeza kuwa Serikali, kupitia wizara husika kwa kushirikiana na wadau wa sekta mbalimbali, inaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayohakikisha wazee wanapata huduma, fursa na nafasi ya kushiriki katika masuala ya kijamii na maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Kitaifa, David Sando, amewataka wazee kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kurithisha vijana maadili mema, uzalendo na uzingatiaji wa sheria.
Amesisitiza kuwa wazee wana wajibu wa kutumia uzoefu wao kukemea vitendo viovu vinavyoweza kuhatarisha amani na kuchangia mmomonyoko wa maadili katika jamii, huku wakiendelea kuwaelekeza vijana katika kuhifadhi tunu za taifa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Farida Mgomi, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini mchango wa wazee katika maendeleo ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha katika maamuzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kongamano hilo limekuwa fursa ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya Serikali na wazee, pamoja na kujadili mikakati ya kuboresha ustawi wao na kuendeleza mchango wao katika kudumisha amani, kuimarisha maadili na kuchochea maendeleo ya taifa.
MWISHO