Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WASANII WATAKIWA KUWA MABALOZI WA ULINZI NA USALAMA WA WATOTO MTANDAONI

Imewekwa: 23 Nov, 2026
WASANII WATAKIWA KUWA MABALOZI WA ULINZI NA USALAMA WA WATOTO MTANDAONI

Na Evelina Odemba – WMJJWMM
Dar es Salaam

Serikali imewataka wasanii kutumia nafasi na ushawishi walionao katika jamii kuwa mabalozi wa ulinzi na usalama wa watoto mtandaoni, kwa kuzingatia haki, maadili na ustawi wa watoto katika kazi mbalimbali za sanaa.

Wito huo umetolewa  leo 22 Novemba 2026   na Afisa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Abel Ndaga, wakati wa mafunzo kwa wasanii kuhusu afua za ulinzi na usalama wa watoto mtandaoni yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao katika kulinda haki na usalama wa watoto wanaposhirikishwa katika kazi za sanaa na maudhui yanayochapishwa kwenye majukwaa ya kidijitali. 

Ndaga amesema wasanii wanapaswa kuhakikisha kazi za sanaa zinazowashirikisha watoto zinazingatia usalama, haki na maadili, badala ya kuwatumia katika maudhui yanayolenga watu wazima.

“Kumekuwa na matukio ya watoto kurekodiwa na wazazi wao na kutumiwa katika maudhui mbalimbali, wakati mwingine wakishirikishwa katika shughuli za kisanaa hadi nyakati za usiku, hali inayoweza kuathiri haki na ustawi wao, ni  muhimu kwa wasanii kutambua mipaka na wajibu wao wanapowashirikisha watoto katika kazi za sanaa ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na rafiki kwa ukuaji na maendeleo yao. ”Amesema Ndaga

Kwa upande wake, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Mwasiti, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua baadhi ya mambo ambayo hapo awali walikuwa wakiyachukulia kuwa ya kawaida katika sanaa, lakini yanaweza kuwa na athari kwa watoto na hata kuathiri kazi zao za kisanaa.

Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Joel Mwakapala, amesema wasanii wamehusishwa katika mafunzo hayo kutokana na nafasi zao kama wazazi na walezi, pamoja na ushawishi walionao katika jamii, ambao unaweza kutumika kueneza elimu kuhusu ulinzi na usalama wa watoto mtandaoni.

Mwakapala amewataka wasanii kushirikiana na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha haki, usalama na ustawi wao wanapotumia teknolojia na kushiriki katika shughuli za sanaa.

slot gacor