WAZEE BUKUMBI WAIPONGEZA SERIKALI.
Na WMJJWM - Mwanza
Wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee Bukumbi mkoani Mwanza wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma na mahitaji yao ya msingi kwa maisha yenye heshima na ustawi.
Shukrani hizo zimetolewa leo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, alipofanya ziara katika makazi hayo ya wazee na watu wasiojiweza, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wazee pamoja na kusikiliza changamoto na mahitaji yao.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wanaoishi katika makazi hayo, MzeeJohn Nguku alisema wazee hao wanaishukuru Serikali kwa kuwajali na kuhakikisha wanapata huduma muhimu katika maisha yao ya kila siku.
“Tunaishukuru Serikali na Wizara yako kwa namna inavyotujali na kutuhudumia bila kuchoka,” alisema Mzee John.
Aidha, aliwapongeza watumishi wa kituo hicho kwa kujitolea kuwahudumia wazee kwa moyo wa huruma, uvumilivu na upendo.
“Ni kazi ngumu wanayofanya watumishi hawa, lakini wanaifanya kwa moyo wa kujitoa.
"Tunawashukuru sana na tunawaombea heri kwa Mungu kwa upendo wanaotuonyesha kila siku,” aliongeza John.
Kwa upande wake, Dkt. Jingu alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wazee na makundi maalum ili kuhakikisha wanapata huduma muhimu na wanaishi katika mazingira salama na yenye heshima.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma katika makazi ya wazee pamoja na vituo vingine nchini ili kuhakikisha wazee na watu wasiojiweza wanapata mahitaji yao ya msingi kama chakula, huduma za afya na makazi bora.
Naye Mfawidhi wa Makazi ya Wazee Bukumbi, Vivian Kaiza aliishukuru Wizara kwa kuendelea kutoa msaada na huduma mbalimbali kwa wazee pamoja na watumishi wanaowahudumia. Alisema msaada huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wazee wanaoishi katika kituo hicho.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha ustawi wa wazee na kuhakikisha wanapata huduma stahiki pamoja na kuthamini mchango wao katika jamii.