Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZAZI, WALEZI WANA WAJIBU KUIMARISHA MALEZI, MAKUZI YA AWALI YA WATOTO- NAIBU WAZIRI MWANAIDI

Imewekwa: 17 Mar, 2025
WAZAZI, WALEZI WANA WAJIBU KUIMARISHA MALEZI, MAKUZI YA AWALI YA WATOTO- NAIBU WAZIRI MWANAIDI

Na WMJJWM,Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Mwongozo wa Taifa wa Uanzishwaji na Uendeshaji wa Vikundi vya Malezi ya Watoto.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amebainisha hayo Machi 15, 2025 mkoani Arusha, wakati wa ziara ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Programu za Malezi mbadala pamoja na Programu ya Uwezeshaji Uchumi wa Familia na Vijana zinazotekelezwa na Shirika linaloshughulika na malezi ya watoto na vijana la 'SOS Children's Village'.

Mhe. Mwanaidi amesema Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuwajengea uwezo Maafisa wa Serikali kuhusu uanzishaji wa vikundi vya malezi chanya katika ngazi ya jamii ili kuimarisha elimu ya malezi ya watoto kupitia vikundi katika ngazi ya msingi ambapo vikundi hivyo ni muunganiko wa wazazi na walezi waliopata mafunzo ya malezi chanya.

“Serikali imeendelea kutumia majukwaa tofauti yakiwemo Majukwaa ya Dini, Mikutano, Makongamano, Michezo, Sanaa, Burudani pamoja na Vyombo vya Habari kutoa elimu ya wajibu wa wazazi na walezi katika malezi ya watoto na familia hivyo Viongozi wa Dini 109 na waumini 35,520 wameweza kufikiwa na kupatiwa elimu hii na tayari tafiti zinaonesha kuna vikundi 3,963 vya Malezi Chanya vimesajiliwa.” Alamesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Vilevile Naibu Waziri Mwanaidi amebainisha kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuzitambua Familia na Watu wa kuaminika na kuwajengea uwezo kwa kuwapa mafunzo ya malezi na matunzo ya Watoto.

“Hadi kufikia Desemba, 2024 jumla ya Watu wa kuaminika 1803 walitambuliwa nchi nzima lakini Pia jumla ya watoto 586 wamepatiwa huduma kupitia Watu wa kuaminika.” ameeleza Naibu Waziri Mwananidi.