Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WATUMISHI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Imewekwa: 10 Sep, 2026
WATUMISHI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Dodoma, Septemba 10, 2026

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Miriam Mmbaga, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao na kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi na utu.

Miriam ameyasema hayo leo, Septemba 10, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha mada kuhusu maadili ya utumishi wa umma kwa watumishi wanaoshiriki kikao kazi kinacholenga kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema, kuzingatia maadili ya kazi ni msingi muhimu wa kujenga utumishi wenye uadilifu, uwajibikaji na ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa watumishi kuwa na nidhamu, kujituma, kushirikiana na kuheshimiana katika kutekeleza majukumu yao.

“Ni muhimu kila mtumishi kutekeleza wajibu wake kwa bidii, ubunifu na uadilifu, kutunza siri za kikazi na taasisi, pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa,” amesema Mmbaga.

Aidha, amewataka watumishi kuendelea kuzingatia misingi ya utumishi wa umma katika mahusiano yao ya kikazi na wananchi, akieleza kuwa mwenendo wa kila mtumishi una mchango mkubwa katika kujenga au kuharibu taswira ya taasisi na Serikali kwa ujumla.

Mmbaga amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinafanyika kwa weledi, heshima, utu na kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.

Amesema nidhamu, bidii, ubunifu, uadilifu na ushirikiano kazini ni miongoni mwa misingi inayoweza kuongeza ufanisi katika utendaji na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na taasisi zake.

slot gacor