KAMISHNA WA USTAWI WA JAMII NCHINI ATOA WITO, KWA WAZAZI / WALEZI KUSIMAMIA MALEZI BORA NA ULINZI WA WATOTO
Na Saidi Saidi WMJJWM - Dar Es Salaam
Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Rehema Kombe ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuzingatia malezi bora, kuwahudumia watoto ipasavyo na kuhakikisha wanawalinda dhidi ya vitendo vya ukatili.
Kamishna Rehema ametoa wito huo Septemba 07, 2026 alipomwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika ziara ya kikazi ya ufuatiliaji na usimamizi wa huduma za Ustawi wa Jamii mkoani Dar es Salaam.
Ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Mwananyamala kwa juhudi na namna unavyotekeleza huduma za Ustawi wa Jamii, hususani utoaji wa huduma jumuishi kupitia Kituo cha One Stop Centre.
Aidha, ameitaka jamii kushirikiana katika malezi na ulinzi wa watoto, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
Kamishna Rehema pia, amesema ulinzi na malezi bora ya watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, jamii na wadau mbalimbali ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye upendo na ulinzi.