Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WARATIBU MADAWATI YA JINSIA WAPIGWA MSASA

Imewekwa: 20 Mar, 2025
WARATIBU MADAWATI YA JINSIA WAPIGWA MSASA

Na WMJJWM- Mwanza

Katika kuhakikisha Ukatili wa Kijinsia unapungua na hata kuisha katika jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaendeleza jitihada za kukabiliana na hilo kwa kutoa mafunzo kwa Waratibu wa Madawati ya Jinsia kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati ili waweze kuyaendesha madawati hayo kama ilivyokusudiwa katika Taasisi hizo.

Akizungumza katika mafunzo kwa Waratibu wa Madawati hayo kwa Vyuo vya Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu Machi 19, 2025 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Rennie Gondwe amesema mafunzo wezeshi kwa waratibu wa Madawati ya Kijinsia kutoka vyuoni yanafanyika ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Akitoa takwimu ya washiriki katika Mafunzo hayo yanayotolewa Jijini Mwanza, Mratibu wa madawati ya Jinsia katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Gift Msowoya alisema kuwa jumla ya washiriki 60 wameweza kupatiwa mafunzo hayo.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo yaligawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza lililowajumuisha washiriki 30 ambao ni viongozi kuoka wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kai lilipatiwa mafunzo Machi 18, 2025 wakati kundi la pili lililowahusisha waratibu wa Madawati ya Jinsia lilipatiwa mafunzo Machi 19,2025 likiwa na washiriki 30.

Aidha miongoni mwa mada zilizofundishwa kwa washiriki hao ni Pamoja na miongozo, uanzishaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati ya Jinsia vyuo vikuu na vyuo vya kati, ukatili wa kijinsia, Rushwa ya Ngono, namna bora ya kuhifadhi taarifa za ukatili katika daftari la usajili Pamoja na ukatili wa miandaoni.