WANAWAKE VIJIJINI WAHIMIZWA KUIMARISHA UZALISHAJI, UCHUMI WA FAMILIA.
Na, WMJJWM – Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewahimiza wanawake wa vijijini kutumia fursa za kiuchumi zilizopo ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha kipato cha familia na kuchangia maendeleo ya taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Anayeishi Kijijini, yaliyofanyika Kijiji cha Vitono, Wilaya ya Kilolo, mkoa wa Iringa, amesema wanawake wana mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula, kilimo, ufugaji, biashara na malezi ya familia.
Amesema pamoja na mchango huo, wanawake wa vijijini bado wanakabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia, masoko, elimu na umiliki wa rasilimali za uzalishaji, hivyo kuhitaji ushirikiano wa Serikali na wadau katika kuwawezesha kiuchumi.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kupitia fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo ya Halmashauri kwa makundi maalum.
Amebainisha pia kwamba, mkoa wa Iringa, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.001 imetolewa kwa vikundi 530 vya wanawake.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Josia Saoke, amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutambua mchango wa wanawake wa vijijini na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali, fursa za kiuchumi na ushiriki wao katika maamuzi ya maendeleo.
Maadhimisho hayo mwaka huu ymeongozwa kaulimbiu isemayo “Mwanamke wa Kijijini: Nguvu ya Uzalishaji, Chachu ya Ustawi na Maendeleo ya Taifa kuelekea Dira 2050,” inayolenga kuimarisha nafasi ya wanawake katika uzalishaji, ustawi wa familia na maendeleo ya Taiifa