WANANCHI TUSHIRIKI MBIO ZA HISANI KUCHANGIA MFUKO WA NGOs - RC SENYAMULE
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Hisani (FUN RUN) za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zitakazofanyika siku ya Jumamosi, Novemba 28, 2026, jijini Dodoma, kwa lengo la kuchangia fedha za kuanzisha mfuko wa pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund – NBF).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Novemba 23, 2026 Senyamule amesema mbio hizo zitaanzia na kuhitimishwa katika Uwanja wa Jamhuri, kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi saa 1:30 asubuhi, ambapo washiriki watapitia maeneo mbalimbali ya jiji, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na Stesheni ya SGR Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa mbio hizo ni fursa muhimu kwa wananchi kuonesha mshikamano na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia ushiriki wao. Senyamule ameeleza kwamba, mbio hizo ni kukusanya fedha zitakazokuwa kianzio cha Mfuko wa pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, utakaosaidia kuimarisha uwezo wa mashirika hayo kutoa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii.
Mfuko huo unatarajiwa kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje na kuwezesha mashirika hayo kuwa na vyanzo endelevu vya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi, hususani katika ngazi ya jamii. Aidha, amewahimiza wananchi, taasisi za umma, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na mashirika mbalimbali kujitokeza kushiriki mbio hizo, akibainisha kuwa kila mshiriki atakuwa sehemu ya jitihada za kujenga sekta imara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Amesema wananchi ambao hawataweza kushiriki mbio hizo wanaweza kuchangia fedha au vifaa ili kusaidia kufanikisha uanzishwaji na uendelevu wa mfuko huo.
Mbio hizo za hisani ni sehemu ya shughuli za Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026, linaloandaliwa na @maendeleoyajamii kwa kushirikiana na @nacongotz