WALIMU WANAWAKE WATAKIWA KUWA MUHIMILI, UTEKELEZAJI DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050 KUPITIA MALEZI NA MAKUZI BORA YA WATOTO
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka walimu wanawake kuwa vinara wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwekeza katika malezi na makuzi bora ya watoto, ili kujenga kizazi chenye maadili, maarifa na ujuzi.
Akizungumza Agosti 1, 2026 wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Walimu Wanawake Tanzania (Tanzania Women Teachers Gala 2026) jijini Dodoma akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Dkt. Gwajima amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia maboresho ya sera, ajira za walimu, ujenzi wa miundombinu na matumizi ya TEHAMA.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali itatoa ufadhili wa masomo kwa walimu 1,223 wa Elimu Maalum, kuwajengea uwezo walimu 3,000 wa ushauri na unasihi, kutoa mafunzo kazini kwa watendaji 5,500 wa elimu, kujenga madarasa 1,360, mabweni 17, nyumba 33 za walimu, vituo 50 vya walimu, pamoja na kuajiri walimu 7,000 ili kuboresha uwiano wa walimu na wanafunzi na kuongeza ubora wa elimu nchini
Aidha, amewapongeza walimu wanawake kwa mchango wao katika kufundisha na kulea watoto, huku akiwahimiza kutumia teknolojia na mbinu za kisasa za ufundishaji. Pia amewataka kuendelea kuwa walinzi wa watoto kwa kutambua na kuripoti viashiria vya ukatili kwa wakati, akisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni msingi wa kujenga rasilimali watu yenye tija na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOTE Forum Tanzania, Mwalimu Sheila Chinja, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuwawezesha walimu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hivyo wataendelea kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha malezi na makuzi bora ya watoto, kuwajenga wanafunzi wenye maadili, maarifa na uzalendo, pamoja na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuinua ubora wa elimu nchin