Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WALEZI WA VITUO VYA WATOTO WAHIMIZWA KUWAELIMISHA WAZAZI.

Imewekwa: 26 Mar, 2026
WALEZI WA VITUO VYA WATOTO WAHIMIZWA KUWAELIMISHA WAZAZI.

Na WMJJWM-Morogoro

Walezi wa watoto wadogo mchana wamehimizwa kutoa elimu ya malezi kwa Wazazi na Jamii kuhusu utambuzi wa viashiria vya tabia hararishi kwa watoto.

Hayo yamesema Machi 25, 2026 na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, David Ntezidyo baada ya kutembelea kituo cha kulea Watoto wadogo mchana cha Little Havard mkoani Morogoro.

Ntezidyo amesisitiza kuwa malezi bora huanza na ushirikiano kati ya mlezi katika Makao ya watoto na mzazi kwani watoto wanapaswa kulelewa katika mazingira yanayowajenga kujitambua, kuwajibika, na kuwa raia wenye maadili mema na uwezo wa kujisimamia wanapokua.

“Walezi mna nafasi ya kipekee sana. Mnakaa na watoto kwa muda mrefu zaidi mchana, hivyo mnaweza kuona tabia zao, mabadiliko yao na hata changamoto wanazopitia. Taarifa hizi ni muhimu kuwafikia wazazi ili waweze kuchukua hatua mapema,” alisisitiza.

Aidha, amewahimiza walezi kutoa mrejesho wa mara kwa mara kwa wazazi kuhusu maendeleo ya watoto wao, ikiwa ni pamoja na viashiria vya tabia zisizofaa, ili kuhakikisha watoto wanakua katika maadili bora na kufanya maamuzi sahihi wanapofikia ujana na utu uzima.

Kwa upande wake, Meneja wa kituo hicho, Lubayna Hamad alieleza shukrani zake kwa wataalamu kutoka Serikalini kwa kutembelea na kutambua juhudi zinazofanywa na vituo vya kulea watoto. Amesema ziara hiyo ni faraja na motisha kwa wahudumu kuendelea kuboresha huduma zao.

“Tutahakikisha tunaendelea kutoa malezi yenye weledi, tukijenga watoto katika msingi wa upendo, mshikamano na maadili mema, ili wawe chachu ya maendeleo ya taifa letu,” amesema Lubayna.

Ziara hiyo inalenga kuona jinsi utoaji wa huduma mbalimbali za ustawi wa Jamii, ikiwemo malezi ya mtoto katika vituo vya kulea Watoto wadogo mchana pamoja na Makao ya Watoto.

MWISHO