UMALITA WARIDHISHWA MIKAKATI YA SERIKALI KUWAENDELEZA KIUCHUMI
Na WMJJWM Dodoma
Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), wameridhishwa na mikakati ya Serikali ya kuwatambua na kuwaendeleza kiuchumi ili watoke kqenye biashara ya kujikimu na kuwa na malengo makubwa.
Hayo yamebainika katika ziara ya umoja huo waliyoifanya katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum leo Oktoba 29, 2026 Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, Mwemyekiti wa UMALITA Havijawa Omary amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa na wao kama sehemu ya wanufaika wamefurahi kujionea miundombinu bora iliyowekwa ili kuwahudumia wananchi.
Amesema wako tayari kumsaidia Rais kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezeka hasa kuhakikisha ustawi na uchumi wa watu.
"Ustawi na uchumi wa watu unaimarika iwapo pia wanakuwa na afya njema. Tuko radhi kutoa shilongi elfu 2 kila siku ili kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya kwa wote kwa sababu kuna baadhi yetu wanakopa hadi mikopo ya kausha damu ili kupata matibabu"
Jessica Kikumbi ambaye ni mmiliki wa Migahawa maarufu ya Kitambaa Cheupe naye amepata nafasi ya kishiriki ziara hiyo ambapo amewasihi Baba na Mamalishe kuitumia fursa ya kutambuliwa na Serikali na kuweka wizara zote mahali pamoja ni ya kipekee hivyo waitumie vizuri kujiimarisha.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Eliakim Maswi amewaeleza UMALITA kuwa, Serikali inaandaa mikakati ya kuwatambua Baba na Mama lishe wote nchini iwe rahisi kuwaratibu na kutumia fursa zilizopo kwa ufanisi.
Maswi amebainisha kwamba Serikali inatambua changamoto za mama na baba lishe nchini ikiwemo kutokuwa na uhakika wa maeno ya biashara, masoko, miundombinu safi, mitaji, afya, lishe na usalama.
Amesema kutokana na changamoto hizo, ni vema kuhakikisha kundi hilo linaratibiwa vizuri na matokeo yake litafanya mambo makubwa hivyo linahitaji kutambuliwa na kujisajili.
"Mnatoa huduma ya chakula na mnatengeneza Ajira, mnaunganisha masoko ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali" amesema Maswi.