Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

UKATILI WA KIJINSIA KATIKA SEKTA YA UTALII BADO NI KIKWAZO CHA MAENDELEO - DKT STERGOMENA TAX

Imewekwa: 11 Mar, 2025
UKATILI WA KIJINSIA KATIKA SEKTA YA UTALII BADO NI KIKWAZO CHA MAENDELEO - DKT STERGOMENA TAX

Waziri wa Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dkt. Stargomena Tax ameitaka jamii kuamka na  kupinga ukatili wa kijinsia kwenye sekta ya utalii kwani licha ya mafanikio ya sekta hiyo, bado wanawake wamekuwa na ushiriki mdogo katika mashirika na makampuni ya utalii ikilinganishwa na wanaume.

Dkt. Stergomena amebainisha hayo katika kongamano la wanawake wa kanda ya Kaskazini Machi 06,2025, Mkoani Arusha.

Ameeleza kwamba  sekta ya Maliasili na Utalii inachangia asilimia 17 ya pato la Taifa, jambo  linalopaswa kupewa kipaumbele cha kipekee na kila mmoja ili kuhakikisha wananchi wengi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi za sekta hii, hivyo kukuza mchango wa sekta hii katika pato la Taifa.

 “Tafiti zinanaonesha kuwa, kazi zinazofanywa na wanawake kwenye sekta ya utalii ni zile zenye ujira mdogo mfano wafanyakazi wa hoteli, migahawa na kumbi za utalii. Hivyo, kuna kila sababu ya kujadili na kupata majibu ya  jinsi gani ya tunaweza kuwainua wanawake  kushiriki na kunufaika na sekta ya utalii.”amesema Dkt Stergomena.

Vilevile Dkt Stergomena ametoa wito kwa jamii nzima kutambua kuwa ujenzi wa Taifa lolote Duniani hauwezekani isipokuwa kwa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume hivyo,  kiwango cha maendeleo kilichokusudiwa ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wanawake na wanaume katika nyanja zote kwa kiwango sawa.

Aidha,Dkt Stergomena  ameipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) kupitia Kituo cha Kitaifa cha Utafiti na Uhifadhi wa Machapisho yanayohusu Wanawake (NWRDC)kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo.