Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA HATUA ZA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Imewekwa: 13 Mar, 2026
TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA HATUA ZA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Na WMJJWM – New York, Marekani

Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kimataifa yanayohusu usawa wa kijinsia na maendeleo, sambamba na kuimarisha juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kutekeleza kikamilifu na kwa ufanisi hatua zilizowekwa katika makubaliano mbalimbali ya kimataifa kuhusu jinsia na maendeleo ambayo nchi imeridhia.

Dkt. Gwajima amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoingia katika makubaliano na maazimio mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo Azimio na Jukwaa la Utekelezaji la Beijing, Mkataba wa Kutokomeza Aina zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinatokomezwa. Miongoni mwa hatua hizo ni utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) wa mwaka 2024/25 hadi 2028/29, unaolenga kupunguza vitendo vya ukatili kwa asilimia 50.

“Kupitia mpango huu, Serikali imeendelea kupanua dawati za jinsia na watoto katika vituo vya polisi, ambapo zaidi ya dawati 420 yameanzishwa nchini kote. Pia imeanzisha vituo jumuishi vya huduma (One Stop Centres) katika baadhi ya vituo vya afya ili kutoa msaada wa kitabibu na kisheria kwa waathirika wa ukatili,” amesema Dkt. Gwajima.

Ameongeza kwamba Serikali imeendelea kutekeleza sheria mbalimbali zinazolinda haki za wanawake na watoto, ikiwemo Sheria ya mtoto pamoja na kuimarisha kampeni na programu za kupambana na vitendo vya ukeketaji pamoja na ndoa za utotoni.

Dkt. Gwajima pia amefafanua kuwa kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 kumewezesha kupanua huduma za msaada wa kisheria kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu, hususan wanawake maskini wa vijijini, wajane na watu wenye ulemavu.